Sh1 bil kumaliza mchezo wa Yanga

Muktasari:

  • KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na ile wa Utendaji ya Yanga zinakutana leo ili kuteta kwa kina juu ya mustakabali wa Uchaguzi wa klabu hiyo na hatma ya Yusuf Manji ndani ya klabu hiyo aliyetangaza kurejea uongozini.

KABLA ya jioni ya leo wanachama na mashabiki wa Yanga watafahamu mbivu na mbichi juu ya bilionea wao Yusuf Manji kama ataendelea kuiongoza Yanga kama Mwenyekiti au la, wakati Kamati ya Uchaguzi wa TFF na ile ya Utendaji ya klabu hiyo zitakapokutana kumaliza utata.

Kikao hicho kitafanyika leo Ijumaa, ikiwa ni siku moja tangu vigogo wa Serikali na Kamati ya Uchaguzi wa TFF kukutana kwa siri mjini Dodoma kujadiliana ishu ya Manji aliyetangaza kurejea Jangwani huku ukiitishwa uchaguzi wa nafasi yake.

Vigogo wa Serikali wakiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Alex Nkenyenge waliitana Dodoma na wajumbe wa kamati hiyo ya TFF.

Lakini unaambiwa iwapo Manji atapigwa chini jumla kupitia kikao hicho ili kuruhusu nafasi yake ya uenyekiti iwaniwe kwenye mchakato wa uchaguzi basi huyo mrithi wake na mabosi wenzake lazima wajipange kubeba mzigo mzito mdani ya klabu hiyo.

Mwenyekiti mpya wa Yanga atakayepatikana Januari 13 lazima aanze kujipanga sasa hasa kuwa na fungu la maana linalokaribia Sh 1 bilioni la kulipa madeni na gharama ambazo klabu inadaiwa ikiwamo na wachezaji wa timu hiyo.

Bosi huyo mpya lazima awe na fedha hizo ili kutuliza hali ya mambo klabu kutokana na ukweli kwamba tangu Manji ajiuzulu Mei 20 mwaka jana, Yanga imekuwa ikinuka ukata na kudaiwa mamilioni ya fedha kila kona.

Mwanaspoti limedokezwa kuwa, Yanga huwa inatumia si chini ya Sh 150 milioni kwa ajili ya kulipa mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo na kwa taarifa zaidi ni kwamba wachezaji wanaidai klabu mishahara zaidi ya miezi minne.

“Novemba hii ikimalizika itatimia miezi mitano wachezaji hawajalipwa mishahara, hapo ni mbali na makocha, na fedha nyingine za kuhudumia timu,” chanzo cha habari ndani ya Yanga kilidokeza Mwanaspoti.
Katika hilo ina maana Yanga hasa mwenyekiti anayekuja basi awe na na kiasi kisichopungua sh 1.5 bilioni kuweza kulipa mishahara mpaka kufika mwisho wa mwezi Januari mwakani wakati uongozi mpya utakapoingia madarakani.

FUNGU LA USAJILI

Achana na fungu hilo la mishahara, eneo lingine ni malipo ya deni la fedha za usajili ambapo deni la sasa ni kiasi kisichopungua Sh 300 milioni kulipa madeni ya wachezaji wa sasa.
Katika eneo hilo hilo, bado Yanga inahitaji kumsajili katika dirisha dogo ambalo ilisharipotiwa na Mwanaspoti kuwa, Manji alishaanza mchakato wa kuweka mzigo mezani ili kuboresha kikosi na inaelezwa zinahitajika kiasi kisichopungua Sh300 mil kukisuka kikosi hicho.

MECHI ZA UGENINI

Kabla ya klabu kufanya uchaguzi Januari 13 mwakani, Yanga itacheza mechi 10, saba zikiwa za ugenini na tatu za nyumbani, kwa hali ilivyo Jangwani kwa sasa ni wazi bosi mpya anayekuja ajipange kwelikweli kwa kusafirisha timu ambayo ni ishu.

Taifa Stars tu ndio imezima upepo wa Yanga mbaya wa fedha, kwani timu imepumua kwa kubaki Dar kucheza mechi za kirafiki, lakini Stars ikimaliza mechi yake Lesotho, Ligi itaendelea na Yanga kuanza na viporo viwili ugenini.

Hizo ni kati ya mechi sita watakazocheza mikoani, mbali na ile ya ugenini dhidi ya Azam itakayopigwa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Katika safari hizo, kila mchezo Yanga inahitaji kutumia kiasi kisichopungua Sh 19 milioni na kwa mechi hizo na maandalizi yake klabu inatarajiwa kutumia si chini ya Sh 130 kumudu kusaka pointi 21 katika mechi hizo.

Gharama hizo zinajumuisha pia usafiri wa ndege katika mechi tatu za mjini Bukoba dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa Novemba 25 na ile ya mapema wiki ijayo dhidi ya Mwadui mjini Shinyanga mbali na mechi ya Prisons Mbeya.