Mane avunja rekodi ya ufungaji

Muktasari:

 

  • Tangu Januari mosi mwaka huu, Mane amekuwa kinara wa kutupia mabao akifunga tisa sawa na kinara wa sasa wa mbio za ufungaji bora wa Ligi Kuu, Sergio Aguero

London, England. Mshambuliaji Sadio Mane ndiye mchezaji Msenegal anayeshikilia rekodi ya kufunga magoli mengi zaidi kwenye Ligi Kuu ya England, baada ya kutupia bao lake la 17 msimu huu dhidi ya Fulham jana.

Mane aliisaidia Liverpool kushinda 2-1 kwenye Uwanja wa Craven Cottage na kuendeleza kiwango chake bora wakati Liverpool ikikwea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Straika huyo sasa ameipita rekodi ya Demba Ba ya kufunga magoli 16 akiwa na Newcastle msimu wa 2011-12, na pia ameipita rekodi yake mwenyewe ya kufunga magoli 10 ya ligi aliyojiwekea msimu uliopita.

Amewafikia pia Harry Kane, Pierre- Aubameyang na mchezaji mwenzake wa Liverpool, Mohamed Salah, wenye magoli 17 kila mmoja wakishika nafasi ya pili katika chati ya vinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Uingereza msimu huu.

Tangu Januari mosi mwaka huu, Mane amekuwa kinara wa kutupia mabao akifunga tisa sawa na kinara wa sasa wa mbio za ufungaji bora wa Ligi Kuu, Sergio Aguero.