Mane: Liverpool tunabeba ubingwa

Muktasari:

  • Kwa sasa Liverpool wapo mbele kwa pointi nne dhidi ya Man City na Mane anaamini kilichotokea huko nyuma watakuwa wameelewa somo, hivyo huu ni wakati wao wa kufanya kweli na kumaliza kiu yao ya miaka 29 ya kubeba ubingwa huo.

LIVERPOOL, ENGLAND.SUPASTAA wa Liverpool, Sadio Mane amewaambia wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, Manchester City tena kwa msisitizo: “Safari hii hatutelezi.”

Mane ana uhakika mkubwa kwamba Liverpool itabeba ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza na kukwepa kile kilichotokea misimu michache iliyopita, ambapo Steven Gerrard aliteleza na kwenye mechi ya Chelsea na kuwafanya Man City kubeba ubingwa mwaka 2014.

Kwa sasa Liverpool wapo mbele kwa pointi nne dhidi ya Man City na Mane anaamini kilichotokea huko nyuma watakuwa wameelewa somo, hivyo huu ni wakati wao wa kufanya kweli na kumaliza kiu yao ya miaka 29 ya kubeba ubingwa huo.

Mane alisema: “Hii sio timu ya watu wa kuharibu. Ubingwa tunachukua.” Tangu tukio la Gerrard limewafanya Liverpool kuwa kituko kwenye mbio za ubingwa ambapo mashabiki wengi wamekuwa wakiamini kwamba hawana uwezo wa kunyakua ubingwa huo, lazima watateleza tu kabla ya msimu kufika mwisho.

Lakini, hilo halipo kwenye akili ya staa huyo wa kimataifa wa Senegal, akisisitiza: “Nina hakika tutakuwa mabingwa wa England. Kila nikiamka, nikienda mazoezini huwa nakuwa na mawazo hayo.”