Manchester United yaweka ubaoni wanaoingia na kuondoka

Friday May 24 2019

 

Manchester, England. OLE Gunnar Solskjaer ameshawatambua wachezaji anaotaka kuwapiga chini Manchester United katika mpango wake wa kukifumua na kukijenga upya kikosi hicho katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Solskjaer alishamwambia makamu mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward wachezaji anaotaka waondolewe kwenye timu, ili kupata nafasi ya kuingiza wapya wa kuja kuboresha kikosi.

Ander Herrera na Antonio Valencia tayari wameshaondoka, huku Matteo Darmian, Marcos Rojo, Juan Mata na Romelu Lukaku wakijiandaa kuondoka kwenye timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.

Lukaku, ambaye alijiunga na Man United akitokea Everton kwa ada ya Pauni 75 milioni miaka miwili iliyopita anasakwa na Inter Milan, ambayo ipo kwenye hatua za mwisho kabisa za kumteua Antonio Conte kuwa kocha wao mpya. Conte alijaribu kumsajili Lukaku alipokuwa huko Chelsea, lakini alizidiwa ujanja wa Jose Mourinho kwa kumsajili na kumleta Man United. Mata anaondoka kama mchezaji huru, wakati Darmian na Rojo watapigwa bei hata kama ni kwa hasara.

Kwenye mpango huyo, Solskjaer amemwambia bosi wake kwamba anataka wachezaji wapya wasiopungua watano kabla ya Julai Mosi.

Miongoni mwa wachezaji ambao Solskjaer anawataka kwenye kikosi chake ni beki wa Leicester City, Harry Maguire, yule wa Napoli, Kalidou Koulibaly, beki wa kulia wa Crystal Palace, Aaron Wan-Bissaka, winga wa Swansea, Daniel James na fowadi wa Lille, Nicolas Pepe. Kocha huyo anamsaka pia staa wa Borussia Dortmund, Jadon Sancho, anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 100 milioni, lakini kwa kushindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, Man United watapata shida sana katika kukamilisha dili la kinda huyo wa Kingereza. Kwenye rada zake yupo kiungo wa PSG, Adrien Rabiot, anayepatikana bure na kiungo wa West Ham United, Declan Rice, ambaye atamgharimu Pauni 50 milioni.

Advertisement

Advertisement