Manchester United yawataka Coutinho, Rakitic kuziba pengo la Pogba

Muktasari:

Taarifa za awali zimedai kuwa Pogba anauzwa Pauni 150 milioni fedha ambazo zinaweza kutumika kuwanunua Coutinho na Rakitic.  

London, England. Manchester United inaripotiwa iko mbioni kuwasajili kwa pamoja nyota wawili wa Barcelona, Philippe Coutinho na Ivan Rakitic.

Man United imewageukia nyota hao kujaza nafasi ya Paul Pogba anayehusishwa na mpango wa kutua Real Madrid majira ya kiangazi.

Mbali na Real Madrid, Juventus inahusishwa na mpango wa kumwania Pogba ambaye tayari ameweka bayana nia ya kuondoka Old Trafford.

Taarifa za awali zimedai kuwa Pogba anauzwa Pauni 150 milioni fedha ambazo zinaweza kutumika kuwanunua Coutinho na Rakitic.

Katika hatua nyingine Arsenal imeingia katika anga za Manchester United kwa kuisaka saini ya Thomas Meunier.

Muda mfupi baada ya Man United kutangaza nia ya kutaka huduma ya mchezaji huyo wa Paris Saint Germain, Arsenal nayo imesema inamtaka katika usajili wa majira ya kiangazi.

PSG imesema ipo tayari kumtoa Meniuer anayecheza nafasi ya beki wa kulia kwa Pauni27 milioni na bonasi.

Kocha wa Arsenal, Unai Emery amevutiwa na beki huyo wa kimataifa wa Ubelgiji na amepania kumsajili majira ya kiangazi.

Awali, iliripotiwa Man United ilitangulia kutuma maombi ya kumsajili mchezaji huyo ikiweka mezani Pauni22 milioni.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer anataka beki wa kuziba pengo la nahodha wake Antonio Valencia ambaye amewekwa sokoni.

Hata hivyo, Emery anaweza kumkosa mchezaji huyo kutokana na kiasi kidogo cha fedha ya bajeti alichopewa.

Meunier amecheza mechi 31 za klabu yake katika Ligi Kuu ya Ufaransa msimu uliopita.