Manchester United kung’oa kibao

Thursday May 16 2019

 

LONDON, ENGLAND.PANGA halikwepeki Manchester United. kocha wa kikosi hicho, Ole Gunnar Solskjaer amekuwa mkali na kusisitiza atawaondoa wachezaji wengi kwenye dirisha lijalo la usajili.

Hata hivyo, unaambiwa hivi kocha huyo huenda akagusa wachezaji wote, lakini si kinda Anthony Martial, ambaye mmiliki mwenza wa timu hiyo, Joel Glazer anamwona kama Pele wa Man United.

Martial kujituma kwake kwenye kikosi hicho kumetiliwa mashaka na makocha wote Jose Mourinho aliyeondoka na huyu wa sasa Solskjaer jambo linalotia wasiwasi mkubwa wa hatima ya Mfaransa huyo kuendelea kubaki Old Trafford msimu ujao.

Hata hivyo, kutokana na kuwa mchezaji kipenzi cha bosi, Martial anaweza kuwa salama. Januari mwaka huu, Martial alisaini mkataba mpya hadi 2023 ambao utamshuhudia akiweka kibindoni Pauni 200,000 kwa wiki.

Makamu Mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward naye anamwona Martial ni silaha ya siku za baadaye. Kipindi kile Mourinho alitaka kumwondoa ili kumleta winga Ivan Perisic, lakini mabosi Glazer na Woodward wakamtaka Martial kwenye timu.

Kutokana na hilo, Kocha Solskjaer atakuwa na orodha yake ya wachezaji kadhaa ambao hataguswa akiamua kuwaondoa kwenye kikosi hicho ili kupunguza bili ya mishahara na kuwanasa wachezaji wengine wapya watakaokuwa na faida kwenye timu.

Ripoti zinadai kuna orodha isiyopungua wachezaji wanane wataachana na maisha ya Man United kwenye dirisha lijalo la usajili, huku ikidaiwa kuna sura tano mpya zitatua hapo kabla ya Julai Mosi watakapoanza mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao.

Wachezaji Antonio Valencia na Ander Herrera hao hawatakuwapo Old Trafford msimu ujao, lakini panga la Ole huenda likapitia pia majina ya mastaa kama Matteo Darmian, Marcos Rojo, Eric Bailly, Juan Mata, Romelu Lukaku na Alexis Sanchez.

Kuna taarifa pia zinazomtaja Paul Pogba kuwa ni miongoni mwa mastaa watakaofunguliwa milango ya kutokea licha ya Bosi Woodward kumtaka mchezaji huyo aendelee kubaki Old Trafford kwa sababu za kibiashara.

Ole hataki mzaha na ndio maana kwenye orodha ya wakali wanaotajwa kwamba watapigwa panga Old Trafford kuanzia sasa wote ni mastaa wakubwa.

Advertisement