Manara atulizwa na Baba yake

Muktasari:

  • Nugaz alisema amepenyezewa kwamba Manara na Paul Makonda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni mashabiki ndakindaki wa Yanga.

MCHEZAJI wa zamani wa Yanga, Sunday Manara ambaye pia ni baba mzazi wa msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara amewataka mashabiki wa Yanga wasiumize kichwa na mtoto wake.
Sunday alisema yeye ndio anamjua vizuri mwanae hivyo wasiwe wanaweweseka na mambo ya kijana wake.
"Haji mimi ndio baba yake mzazi kwahiyo msikeleke naye, yule katokea katika nyumba yangu na namjua vizuri," alisema.
Baada ya kuyasema hayo shangwe ziliibuka ukumbini hapa wakimshangilia baba huyo wakati akizungumza.
Wakati huo huo mshereheshaji mwingine wa shughuli hii, Antonio Nugaz alisema amepenyezewa kwamba Manara na Paul Makonda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni mashabiki ndakindaki wa Yanga.
"Licha ya kwamba mkuu wa mkoa Makonda ni mwanachama wa Simba pamoja na Manara, nimeambiwa hawa ni wenzetu na ndio maana wamekuwa hawawezi kufanya kitu bila kututaja taja," alisema Nuggaz.
Manara amekuwa akitoa vijembe vya utani mara kwa mara kwa watani wao wa jadi Yanga.