Manara ajibu maswali mawili kupokonywa usemaji na MO

Muktasari:

MO alisema  uamuzi huo umelenga kupata idadi kubwa ya mashabiki watakaojitokeza uwanjani siku hiyo ili kuiunga mkono timu hiyo kwenye mechi hiyo ya hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya  Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘MO’ kuzungumzia kuhusu mechi ya Simba na Alh Ahly, kumeibuka mjadala kwenye mitandao ya kijamii wakihoji huenda Ofisa Habari wa klabu, Haji Manara ambaye huwa mara nyingi huzungumza ikawa amewekwa benchi katika nafasi hiyo.

Hata hivyo Manara ameandika kwenye ukurasa wake wa Istagram akitolea ufafanuzi jambo hilo.

Aliandika swali ikifuatiwa na ufafanuzi akisema “Kwa nini Haji hakuwepo  wakati Mwenyekiti wetu wa Bodi ya Simba alipokuwa akizungumza?

Jibu:  Nilikuwepo na waandishi waliniona ila boss wangu alinipa jukumu la kikazi wakati press ikiendelea.

“ Why  sijafanya promo ya game yetu dhidi ya Ahly?

Jibu: Guys Mwenyekiti akishaongea huwezi kuweka lako katika siku hiyo hiyo, ni kukosa weledi ambao haupaswi kufanywa na mtu wa caliber yangu!!!

Awali, uongozi wa Simba ulitangaza bei ya kiingilio kwenye mchezo baina ya timu yao na Al Ahly, Jumanne ijayo ambacho kitakuwa ni Sh2000 kwa jukwaa la mzunguko.

MO alisema  uamuzi huo umelenga kupata idadi kubwa ya mashabiki watakaojitokeza uwanjani siku hiyo ili kuiunga mkono timu hiyo kwenye mechi hiyo ya hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika.