Manara: Simba tumeshtushwa, Wanasimba tulieni

Thursday October 11 2018

 

Dar es Salaam. Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara na mmiliki wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ zimewashtua, lakini bado wanaamini jeshi la polisi litafanya kazi yake.

Manara amesema taarifa ya MO kupata matatizo imemshtua kila mmoja na kwamba bado wanaliachia jeshi la polisi kufanya kazi ya kumpata mwekezaji wao.

Amesema kwa sasa Wanasimba wawe watulivu wakiliachia jeshi la polisi kufanya kazi yake na kwamba wanaamini MO atapatikana akiwa hai.

Amesema wako katika hudhuni kubwa kutokana na jana tu walikuwa naye katika kikao cha bodi ya wadhamini akiwa na furaha wakati wote.

Leo asubuhi, MO aliyekuwa akielekea kwenye hotel ya Colosseum, alitekwa na wazungu wawili na Kamanda Lazaro Mambosasa alieleza kuwashikilia watu watatu.

"Asubuhi ya leo wazungu wawili walikuwa na gari aina ya suff. Kulikuwa na magari mawili, gari moja lilikuwa ndani na lingine lilikuwa nje, gari la ndani liliwasha taa ghafla na lile lililokuwa nje likaingia na kwenda kupaki karibu na gari la MO Dewji lililokuwa limepaki na MO akiwa ndani ya gari hilo," amesema Mambosasa leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

"Wazungu wawili wakatoka na kumbana MO Dewji baada ya kutoka ndani ya gari lake, na kisha kumpakia katika gari lao aina ya suff na kuondoka naye," alisema Mambosasa.

Advertisement