Man United waambiwa Sancho mwisho Agosti 10

Muktasari:

Man United imekuwa ikisaka huduma ya Sancho kwa muda mrefu na mwenyewe amekuwa akitaka kwenda kucheza kwenye klabu hiyo

IMEISHA hiyo. Pauni 108 milioni, Agosti 10 la pambaneni na hali zenu. Hicho, ndicho Borussia Dortmund inachoripotiwa kuwaambia Manchester United kwenye mipango yao ya kumsajili Jadon Sancho.

Miamba hiyo ya Ujerumani, Borussia Dortmund inafahamu Man United kwa muda mrefu wamekuwa wakitajwa kutaka kunasa saini ya winga huyo wa Kingereza, Sancho lakini imewapa masharti mawili ya kufanya ndani ya mwezi mmoja, wakishindwa imekula kwao.

Dortmund imewaambia Man United kama kweli wapo siriazi, wanamtaka Sancho basi wahakikishe wanafanya mchakato wa kumsajili hadi itakapofika Agosti 10, tofauti na hapo, dili hilo linafungwa na hawatakuwa tayari kumuuza mchezaji wao.

Wababe hao wa Bundesliga hawataki kusumbuka na usajili kwa dirisha lote la uhamisho wa majira ya kiangazi, hivyo wanawataka Man United kujikusanya mapema na kukamilisha dili hilo la kumsajili Sancho kabla ya kufikia Agosti 10.

Mchezaji huyo wanasema anauzwa Pauni 108 milioni.

Dortmund walisema mchezaji wao kuendelea kuhusishwa kwenye usajili kunamfanya ashindwe kutuliza akili yake uwanjani huku wakitaka pia muda wa kutosha wa kutafuta mrithi wake kabla ya dirisha kufungwa na kuanza kwa msimu ujao.

Sancho ni moja ya wachezaji wanaoshika namba moja kwenye rada za usajili wa Man United na Kocha Ole Gunnar Solskjaer amepanga kunasa kikosi chenye mastaa wengi vijana, wenye vipaji na njaa ya mafanikio.

Kwa mujibu wa gazeti maarufu la Ujerumani la Bild, Dortmund wameshikilia mpini, wakipanga mwisho wa usajili wa staa wao, Sancho jambo linalowaweka Man United kwenye presha kubwa katika mchakato wao wa kunasa huduma ya mchezaji huyo.

Wameweka wazi hawataketi kitako kusikiliza ofa isiyofikia Pauni 108 milioni, ambayo wao ndio wanaamini inastahili kwenye kumpiga bei supastaa wao huyo matata kabisa.

Kumekuwa na ripoti huku Ujerumani kwamba Sancho ameshafikia makubaliano binafsi na Man United na kwamba kilichobaki kwenye dili hilo ni makubaliano ya ada ya uhamisho baina ya klabu hizo mbili.