Man United kulipa deni leo kwa Brighton?

Muktasari:

Mwaka jana katika raundi ya 12, Manchester United wakiwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Old Trafford kabla ya janga la virusi vya corona  waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Brighton.

Brighton, England. Ligi Kuu England inatarajiwa  kuendelea leo kwa mchezo mmoja utakazoikutanisha Brighton & Hove Albion dhidi ya  Manchester United.
Mchezo huo, unatarajiwa kwa na ushindani kutokana na Brighton kuwa katika vita ya kujihakikishia nafasi ya kusalia katika Ligi huku Manchester United wakiwa na kiu ya kumaliza msimu wakiwa katika nafasi nne za juu 'Top Four'.
Kocha wa Brighton, Graham Potter alisema  hawana mawazo kuwa ni pointi ngapi wakiwa nazo wanakuwa salama ila kilichopo mbele
yao ni kuhakikisha wanafanya  vizuri katika michezo iliyosalia ili msimu ujao washiriki kwa mara nyingine tena Ligi Kuu England.
"Bado tupo katika mapambano, tuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu ili kuhakikisha tunasalia katika Ligi.
Hii Ligi ni ngumu kwa sababu kila timu imekuwa na ubora na wachezaji wenye uwezo wa kufanya lolote dhidi yako," alisema Potter.
Kocha wa Manchester United,  Ole Gunnar Solskjaer alisema  kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kila mwaka ni jambo jema ambalo kila timu imekuwa ikiliota na wachezaji wakilipenda.
"Kuna timu nyingi ambazo zinahitaji nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, tunatakiwa kufanya vizuri kwenye kila mchezo ambao utakuwa mbele yetu," alisema Solskjaer
Manchester United wapo nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu England wakiwa na pointi 49 katika michezo 31, wapinzani wao katika mchezo wa leo, Brighton wenyewe wana pointi 33 wapo nafasi ya 15.