Man United inasubiri wa kumnyoosha

Muktasari:

Hatua ya nusu fainali inatarajiwa kuchukua nafasi Agosti 16 na 17 ambapo mshindi kati ya Wolves na Sevilla atakuwa anakwenda kukutana na United mchezo ambao utapigwa katika Uwanja wa Stadion Koln huko nchini Ujerumani.

MANCHESTER, ENGLAND. MASHINDANO ya Europa League yaliendelea jana Jumatatu ambapo kulikuwa na michezo miwili ya hatua ya robo fainali na wababe wa soka kutoka England, Manchester United imetinga hatua ya nusu fainali baada ya kuibamiza FC Koebenhavn kipigo cha bao 1-0.

Katika mchezo huo United ilijipatia bao lake kupitia kiungo wake Bruno Fernandes kwa njia ya penalti dakika ya 95, baada ya bao la Mason Greenwood alilofunga dakika ya 45 kukataliwa.

Baada ya mchezo huo mchezaji wa United, Bruno Fernandes aliweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi ikiwa ni jumla ya mabao 21, hakuna mchezaji yeyote ambaye amefikia idadi hiyo ndani ya michuano hiyo ya Europa.

Mchezo mwingine ulikuwa kati ya Inter Milan dhidi ya Bayer Leverkusen ambapo Inter ilifanikiwa kushinda kwa mabao 2-1 na kufanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali.

Mabao ya Inter yalifungwa na Nicolo Barella aliyeingia kambani dakika ya 15, kabla ya Romelu Lukaku kupigilia msumari wa pili dakika ya 21, huku bao pekee la Leverkusen likifungwa na nyota anayewindwa sana na Chelsea Kai Havertz dakika ya 21.

Leo pia kutakuwa na michezo miwili ya mwisho ya hatua hiyo, Shakhtar Donetsk

itacheza dhidi ya FC Basel saa 4:00 usiku , huku Wolverhampton Wanderers itakuwa na kibarua mbele ya wababe wa Hispania Sevilla, mchezo unatarajiwa kupigwa sa 4:00 usiku.

Hatua ya nusu fainali inatarajiwa kuchukua nafasi Agosti 16 na 17 ambapo mshindi kati ya Wolves na Sevilla atakuwa anakwenda kukutana na United mchezo ambao utapigwa katika Uwanja wa Stadion Koln huko nchini Ujerumani.

Pia mshindi wa mchezo kati ya Sevilla na Shakhtar Donetsk atakwenda kukutana na Inter Agosti 17, katika dimba la Dusseldorf Arena huko huko Ujerumani.