Man United ina hela Man City, Liverpool zote zinasubiri

Muktasari:

Man United, inayonolewa na Ole Gunnar Solskjaer, imeripotiwa imeingiza mapato ya Pauni 627.1 milioni kwa msimu uliopita, ikiwa ni karibu Pauni 100 milioni zaidi ya kile ambacho Man City na Liverpool ilivuna kwa msimu huo wa 2018-19.

LONDON ,ENGLAND . KWENYE ligi ya mkwanja, hakuna timu yoyote kwenye Ligi Kuu England inayotia mguu mbele ya Manchester United.

Man United ni watu na pesa zao, wakizifunika timu za Ligi Kuu England kwa miaka 23 mfululizo licha ya kushindwa kutamba ndani ya uwanja kwa miaka ya karibuni.

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu, Man United wapo nafasi ya tano huko, wameachwa nyuma kwa pointi 27 na vinara Liverpool, lakini kwenye ligi ya pesa, miamba hiyo ya Old Trafford, inazidiwa na timu mbili tu, tena sio za England.

Timu zinazoizidi Man United kwa mkwanja mrefu ni Barcelona na Real Madrid, ambazo zinaripotiwa zilikusanya mapato mengi kwa msimu uliopita kuliko wakali hao wa Old Trafford.

Man United, inayonolewa na Ole Gunnar Solskjaer, imeripotiwa imeingiza mapato ya Pauni 627.1 milioni kwa msimu uliopita, ikiwa ni karibu Pauni 100 milioni zaidi ya kile ambacho Man City na Liverpool ilivuna kwa msimu huo wa 2018-19.

Huko kwenye Ligi Kuu England, Man City wanashika nafasi ya pili kwa kukusanya mkwanja mrefu, walipovuna Pauni 538.2 milioni, lakini wakishika nafasi ya sita kwa Ulaya, wakiwa mbele kwa nafasi moja dhidi ya mahasimu wao kwenye mbio za ubingwa, Liverpool, waliokusanya mapato ya Pauni 533 milioni.

Man United imekuwa ikitajwa kuwa klabu tayari na kuongoza kwenye orodha hiyo ya timu zenye pesa ndefu, tangu Deloitte walipoanza kutoa jarida lao la Money League mwaka 1997.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya kipesa wanaamini kwamba si muda mrefu, Man United itaenguliwa kwenye kilele hicho cha kuwa na mkwanja mrefu kutokana na mambo yao yanayoendelea uwanjani.

Kinachoelezwa, Man City ndio watakaowaondoa Man United kileleni kwenye ligi ya mkwanja. Deloitte inafichua kutakuwa na upungufu wa mapato kati ya Pauni 560 milioni hadi Pauni 580 milioni kwa msimu huu, kutokana na klabu hiyo kushindwa kuwamo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa pili.

Timu nyingine inayotishia kuwaondoa Man United kwenye kilele cha pesa ni Liverpool. Wababe hao wa Anfield wanacheza soka tamu kabisa kwa sasa na jambo hilo litawafanya kubeba mataji mengi yatakayowafanya kuvuna mkwanja mrefu.

Barcelona ndio klabu iliyovuna pesa ndefu zaidi kwa msimu huo, wakati ilipoweka kibindoni Pauni 741 milioni na Real Madrid wanashika nafasi ya pili kwa kuingiza kipato cha Pauni 667.5 milioni.

Tottenham waliboresha kipato chao baada ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, hivyo wanashika nafasi ya nane huko Ulaya wakiwa wameingiza kipato cha Pauni 459.3 milioni na Chelsea wapo kwenye nafasi ya tisa wakiwa wameweka kibindoni kipato cha Pauni 452.2 milioni.

Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich walishika namba nne na Paris Saint-Germain walishika namba tano, huku Juventus wakikamilisha 10 bora na hakukuwa na nafasi yoyote kwa Arsenal katika hizo nafasi 10 za timu zenye mkwanja mrefu huko Ulaya.