Man United : Ulikuwa ni mgomo au bahati mbaya?

Muktasari:

  • Mourinho pia alijulikana kama mmoja kati ya makocha bora na waliofanikiwa kwenye soka katika nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa na klabu za Chelsea, Real Madrid, Porto ya kwao Ureno na nyinginezo.

MANCHESTER United imebadilika sana, muda mfupi tu tangu kuondoka kwa kocha wake, Jose Mourinho.

Ilikuwa ikifanya vibaya licha ya kuwa na kikosi kipana au kama wengine wanavyosema ‘kinene’, ikiwa pia na baadhi ya wachezaji bora zaidi duniani.

Mourinho pia alijulikana kama mmoja kati ya makocha bora na waliofanikiwa kwenye soka katika nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa na klabu za Chelsea, Real Madrid, Porto ya kwao Ureno na nyinginezo.

Lakini muda wake Old Trafford ulionekana kuwa mbovu, licha ya kusajili vyema, ikiwa ni pamoja na mchezaji aliyekuwa akishikilia rekodi ya kuwa ghali zaidi, Paul Pogba, ambaye Sir Alex Ferguson alimtoa kwa Juventus bure akiwa tineja, kabla ya Mourinho kuja kumnunua kwa bei ghali sana.

Mreno huyo alikuwa na kikosi kizuri, lakini akawa anafanya vibaya kwenye ligi, akifungwa na kutoa sare badala ya kushinda kwa sana. Hata hivyo, leo hii ni wachezaji wal wale, kikosi kilekile kipo chini ya kocha mpya wa muda kutoka Norway, Ole Gunnar Solskjaer kinachofanya vizuri.

Kwa wastani mechi zote imefanya kadiri ambavyo haikutarajiwa na sasa Solskjaer amekuwa kocha bora kwa mwezi Februari, lakini pia mchezaji wake, Marcus Rashford amechaguliwa kuwa bora zaidi Januari.

Nimebaki kujiuliza kulikoni? Wachezaji wa Man United walikuwa na mgomo baridi kumbeza na kumwangusha bosi wao au ilikuwa ni bahati mbaya tu walikuwa wakishindwa vile.

Nilipata kuandika juu ya Mourinho kugombana na wachezaji wake, kuwakosoa hadharani na hata kumnunia aliyekwenda nyumbani (Anthony Martial) kwa ajili ya kumsaidia mkewe wakati akijifungua na kumkasirikia Pogba uwanjani waziwazi na kufika kumtupa benchi.

Leo hii kaondoka Mourinho, ushindi umerudi maana hadi nilipokuwa naandika Jumamosi asubuhi, katika alama 12 zilizokuwa mbele yao, walifanikiwa kutwaa 10, tena wakishinda dhidi ya moja ya timu bora sita – Tottenham Hotspur, lakini pia dhidi ya wagumu Newcastle United na Brighton pamoja na kwenda sare na Burnley, japokuwa ilikuwa nusura Mashetani Wekundu wakanyagwe.

Rashford alikuwa akibaniwa sana na Mourinho ambaye alifika mahali akataka kumuuza sambamba na Martial, lakini Makamu Mwenyekiti Mtendaji, Ed Woodward akamkatalia, maana kwa umri wake wa miaka 21 ni hazina kubwa, tofauti na alivyotaka Mourinho kusajili wachezaji wenye umri wa miaka 30 au katika eneo hilo.

Kwa mwendo ilionao sasa, na kama itashikilia kasi hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kumaliza ndani ya nne bora, na itazipa wakati mgumu Arsenal na Chelsea, wakati ambapo Liverpool na Manchester City zikiwa katika wakati bora wa kufuzu kwa nne bora kama si kutwaa ubingwa.

Solskjaer anasema lengo yake si kumaliza ndani ya nne bora na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) bali kutwaa ubingwa.

Mourinho alifika mahali alisema kwamba kumaliza ndani ya nne bora ni ngumu, lakini ajabu ni kwamba wachezaji ni hao hao ambao leo hii wamebadilisha mtazamo na kutaka kunyakua ubingwa.

Kipimo halisi kwa Solskjaer, hata hivyo, kitakuwa kwenye mechi dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) katika UCL Jumanne hii.