Man City yavunja rekodi ya karne

Muktasari:

Juzi City iliichapa Watford mabao 2-1 ugenini pale Vicarage Road kupitia Leroy Sane na Riyad Mahrez huku la Watford likifungwa na kiungo Mfaransa, Abdoulaye Doucoure. Kwa kufanya hivyo kuna rekodi imeivunja.

LONDON,ENGLAND.AWALI, ilidhaniwa maisha yangekuwa magumu kwa Pep Guardiola katika Ligi Kuu ya England, lakini sasa imebainika maisha ni rahisi tu kwa Mhispaniola na timu yake ya Manchester City, inatisha kama njaa.

Juzi City iliichapa Watford mabao 2-1 ugenini pale Vicarage Road kupitia Leroy Sane na Riyad Mahrez huku la Watford likifungwa na kiungo Mfaransa, Abdoulaye Doucoure. Kwa kufanya hivyo kuna rekodi imeivunja.

City sasa imefunga mabao 45 katika Ligi Kuu ya England huku ikiruhusu nyavu zake kuguswa mara saba tu. Tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa baada ya mechi 15 tu ni mabao 38 na hiyo ni rekodi kwa timu yoyote ile ya Ligi Kuu kwa kipindi cha miaka 125 iliyopita.

Mara ya mwisho kwa timu kubwa kuwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ilikuwa ni katika msimu wa 1892-93 wakati Sunderland ilipojikuta ikiwa na tofauti ya mabao 39 baada ya mechi 15.

Huu ni mwendelezo wa ubabe wa kikosi cha Guardiola, ambapo msimu uliopita kiliweka rekodi kibao wakati kikitwaa ubingwa. Kwanza kabisa kilifikia rekodi ya Manchester United ya kutwaa ubingwa mapema msimu wa 2000/01 wakati kilipotwaa ubingwa ikiwa na mechi tano mkononi.

City pia ilichukua ubingwa ikiwa na tofauti kubwa ya pointi na timu iliyoshika nafasi ya pili, baada ya kumaliza ikiwa na tofauti ya pointi 19. Awali, timu ambayo iliwahi kuchukua ubingwa kwa tofauti kubwa ya pointi ilikuwa Manchester United ambayo msimu wa 1999/00 ilichukua ubingwa kwa tofauti ya pointi 18 mbele ya Arsenal.

City pia iliweka rekodi ya kushinda mechi 18 mfululizo kati ya Agosti 26 iliposhinda dhidi ya Bournemouth hadi Desemba 27 iliposhinda dhidi ya Newcastle United. Kwa kufanya hivyo ilivunja rekodi ya kushinda mechi 13 mfululizo ndani ya msimu mmoja iliyowekwa na Arsenal msimu wa 2001/02 huku pia ikiwekwa na Chelsea msimu wa 2016/17. Lakini, zaidi ikavunja rekodi ya kushinda mechi 14 mfululizo iliyowekwa na Arsenal kati ya Februari na Agosti 2002.

City pia ilifikia rekodi ya Chelsea ya kushinda mechi 11 mfululizo za ugenini. Chelsea ilikuwa imeweka rekodi hiyo kuanzia Aprili 6, 2008 mpaka Desemba 7. Pia, iliweka rekodi ya kumiliki mpira kwa asilimia nyingi zaidi katika pambano la ugenini kwenye historia ya Ligi Kuu ya England wakati ilipomiliki kwa asilimia 82.13 dhidi ya Everton. City pia iliweka rekodi ya kuzifunga timu zote 19 za Ligi Kuu ya England msimu uliopita. Kwa kufanya hivyo ilikuwa timu ya tatu kufanya hivyo, baada ya Man United kufanya hivyo msimu wa 2010/11 na Chelsea kufanya hivyo msimu wa 2005/06.

Wababe hao pia waliweka rekodi ya kuwa nyuma katika mechi kwa dakika 153 tu ambazo ni kidogo zaidi ndani ya msimu mmoja. Pep pia aliweka rekodi ya kuwa kocha bora wa mwezi mfululizo wakati akifanya hivyo kwa miezi minne mfululizo. Ilikuwa ni kuanzia Septemba hadi Desemba, mwaka jana.

Wakati City iliposhinda mabao manne dhidi ya West Ham ilifikisha mabao 102 katika mechi 35 hivyo, kuwa timu iliyofikisha mabao 100 kwa haraka zaidi ndani ya msimu mmoja. Lakini, ilikuwa ni kwa mara ya nne kwa timu kufunga mabao 100 England. Chelsea ilikuwa imefanya hivyo msimu wa 2009/10 wakati Man City na Liverpool zilifanya hivyo msimu wa 2013/14.