Man City yatoa kipigo cha mbwa kokoko kwa Southampton

Monday November 5 2018

 

Manchester, England. Timu ya Manchester City imeonyesha dhamira ya kutaka kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kishindo baada ya jana usiku kuisambatisha kwa mabao 6-1 Southampton.

Ushindi huo umeiwezesha Man City kujikita kileleni ikiwa pointi mbili juu ya Chelsea na Liverpool zote zikiwa zimecheza mechi 11.

Man City ambayo msimu uliopita ilitwaa ubingwa huo ikiweka rekodi ya kufikisha pointi 100 inawezekana msimu huu ikaivunja rekodi hiyo kutokana na mwenendo iliyonayo.

Katika mchezo huo, Man City ilianza kuhesabu bao la kwanza katika dakika ya sita baada ya mlinzi Wesley Hoedt kujifunga wakati akijaribu kuokoa krosi iliyochongwa na Leroy Sane.

Mshambuliaji mahiri kutoka Argentina, Sergio Aguero aliiongozea Man City bao la pili dakika ya 12 akiiwahi krosi ya Raheem Sterling na dakika tatu baadaye David Silva akaipa bao la tatu.

Wageni walifanikiwa kujipatia baoa la kufutia machozi katika dakika ya 30 kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Danny Ings iliyotolewa na mwamuzi baada ya mchezaji huyo kuwekwa chini na Ederson ndani ya 18.

Wakati timu hizo zikijiandaa kwenda mapumziko Sterling akaifungia Man City bao la nne katika dakika ya pili ya muda wa ziada na kukifanya kikosi hicho cha Pep Guardiola kuongoza kwa mabao 4-1 baada ya kukamilisha dakika 45.

Licha ya kuwa na mabao hayo bado Man City waliendelea kusaka mabao katika kipindi cha pili ambacho walikitawala kwa kiasi kikubwa na Sterling akafunga bao la tano dakika 67 kabla ya Sane kukamilisha karamu ya mabao alipofunga la sita dakika ya 90.

Kocha Guardiola alisema ushindi huo utawarejeshea kujiamini wanapoelekea katika michuano ya Ulaya, lakini akarejea kumfagulia Sterling akisema amekuwa chachu ya mabao ya klabu hiyo.

Sterling chipukizi wa England mwenye miaka 23 ametoa asisti kwa zaidi ya nusu ya mabao ambayo Man City imeyafunga msimu huu, katika kila mchezo amekuwa ama akifunga au kutoa pasi za mwisho karibu kila mchezo.

 

Advertisement