Man City yataja usajili wake ujao

Muktasari:

Taarifa zilizopatikana, Man City inataka kusajili kiungo wa kati, beki wa kati na beki wa kulia katika dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER City imeshaweka wazi wachezaji inaowataka kwenye dirisha hili, Rodri, Harry Maguire na Aaron Wan-Bissaka huku ikifichua kutakuwa na panga litapita Etihad kusafisha wachezaji wasiohitahija kusafisha njia.

Kocha Pep Guardiola anataka kuleta nyota wengine ili kuwa na njaa upya baada ya kubeba mataji matatu msimu uliopita, walipobeba Ligi Kuu England, Kombe la Ligi na Kombe la FA.

Nahodha wa Man City, Vincent Kompany ameshaaondoka kwenye timu hiyo na imeelezwa kuna mastaa wengine kibao wa kikosi cha kwanza watafunguliwa mlango wa kutokea katika kikosi hicho.

Taarifa zilizopatikana, Man City inataka kusajili kiungo wa kati, beki wa kati na beki wa kulia katika dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.

Kwa sababu Fernandinho umri umeshaanza kumtupa mkono akiwa na miaka 34 kwa sasa, Man City sasa inampigia hesabu staa wa Atletico Madrid, Rodri ikitaka akachukue nafasi huko Etihad na imeshakubali kulipa Pauni 62 milioni zilizobainishwa kwenye mkataba wa mchezaji huyo.

Staa mwingine wanayemsaka ni kiungo wa Lyon, Tanguy Ndombele na wa Real Madrid, Marcos Llorente.

Kwenye beki wa kati, chaguo lao la kwanza ni Maguire wakitaka akazibe pengo la Kompany, huku beki wa kulia wanamfukuzia Wan-Bissaka.

Wanamtaka pia beki wa kushoto, wakimpigia hesabu Ben Chilwell ili kuachana na watu kama Benjamin Mendy, Danilo, Nicolas Otamendi na Fabian Delph.