Man City ya 2019 ilivyofunika ubingwa wote wa kibabe England

Thursday May 16 2019

 

LONDON, ENGLAND.HABARI ndiyo hiyo. Manchester City ya Pep Guardiola iliyobeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2018-19 ni bora kuliko timu yoyote iliyowahi kunyakua ubingwa wa ligi hiyo, kwa mujibu wa takwimu zinavyosoma.

Man City imebeba ubingwa huo ikikusanya pointi 98 baada ya vuta nikuvute dhidi yake na Liverpool katika mbio za ubingwa huo ambapo kikosi hicho cha Jurgen Klopp chenye maskani yake Anfield kilikomea kwenye kukusanya pointi 97.

Ubingwa huo wa Man City umefunika awamu nyingine zote ambazo klabu za ligi hiyo zilinyakua taji hilo kibabe. Kuanzia ile Manchester United iliyobeba mataji matatu mwaka 1999, hadi ile Arsenal iliyocheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza mechi na kubeba ubingwa huo wa ligi mwaka 2004 na Chelsea ya Jose Mourinho iliyokuwa moto mwaka 2005.

Wababe hao wote, Man United (1999), Arsenal (2004) na Chelsea (2005) ubingwa wao haufikii huu wa kibabe zaidi wa Man City iliyotwaa msimu huu. Takwimu zinaweka hilo bayana.

Kwa kuanzia ile Man United iliyobeba mataji matatu kwa msimu mmoja mwaka 1999. Kikosi hicho kilichokuwa chini ya Sir Alex Ferguson, kwa msimu huo kwenye mechi 38 ilizocheza, ilishinda 22, sare 13 na kuchapwa mara mbili, huku ikiwa na tofauti ya mabao 43 kwenye yale ya kufunga kutoa ya kufungwa na msimu wote ilikusanya pointi 79.

Arsenal ile isiyoshindika na kucheza msimu wote bila ya kuonja machungu ya kupoteza mechi hata mara moja, kwenye mechi 38 ilizocheza, ilishinda 26 na sare 12. Arsenal hiyo iliyokuwa chini ya Kocha Arsene Wenger ilikuwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa 47 na ilimaliza msimu ikiwa na pointi 90.

Chelsea ya Mourinho ya mwaka 2005 ambayo ililiteka soka la Ligi Kuu England, yenyewe kwenye mechi 38 ilizocheza, ilishinda mara 29, sare nane na ilipoteza mechi moja tu. Ilikuwa na wastani wa mabao 57 ya kufunga na kufungwa, huku ilimaliza msimu na kubeba ubingwa baada ya kukusanya pointi 95.

Inakuja Man City ya msimu huu, ambayo imebeba ubingwa baada ya kukusanya pointi 98. Kikosi hicho cha Guardiola, katika mechi zake 38 ilizocheza msimu huu, imeshinda mara 32, sare mbili na imepoteza mechi nne. Man City imekuwa na wastani wa tofauti ya mabao 72 kutoka yale ya kufunga na kufungwa, huku ikiwa na wastani wa ushindi wa asilimia 84.2 na kujibebea taji lake kwa kufikisha pointi 98.

Advertisement