Man City mabingwa England, Liverpool tabu!

Sunday May 12 2019

 

By LONDON, ENGLAND

Kikosi cha Manchester City ndio mabingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2018-19 baada ya kuwachapa Brighton 4-1 katika mchezo wa mwisho uliopigwa leo Jumapili na kuwaachia vumbi Liverpool. Shukrani kwa mabao ya Sergio Aguero, Aymeric Laporte, Riyad Mahrez na Ilkay Gundogan.

Man City na Liverpool zilikuwa zikimenyana jino kwa jino kwenye mbio za ubingwa huo, ambapo Pep Guardiola na kikosi chake hicho ametangaza ubingwa kwa tofauti na pointi moja tu dhidi ya Jurgen Klopp baada ya kuichapa Wolves 2-0 uwanjani Anfield.

Liverpool imekuwa timu ya kwanza kwenye historia ya Ligi Kuu England kupoteza mchezo mmoja msimu mzima na kushindwa kubeba ubingwa, huku Man City ikiwa timu ya kwanza kutetea taji hilo ndani ya muongo mmoja uliopita. Man City imebeba ubingwa kwa kukusanya pointi 98 katika mechi 38, wakati Liverpool imekusanya pointi 97.

Huko Anfield, mabao mawili ya Sadio Mane yalitosha kuipa ushindi Liverpool katika mchezo wao wa mwisho licha ya kwamba mambo hayakuwa mazuri kwao baada ya ubingwa kubebwa na wababe wa huko Etihad. Liverpool sasa inaendelea kusubiria kubeba taji hilo kwa miaka mingi zaidi.

Katika mechi nyingine zilizopigwa kwenye siku hiyo ya kumaliza msimu, Arsenal iliichapa Burnley 3-1 ugenini, Pierre-Emerick Aubameyang akifunga mbili, wakati Crystal Palace ilijipigia Bournemouth 5-3, huku Newcastel United ikiishinda 4-0 Fulham ugenini. Mechi hizo, uwanjani King Power tu ndiko ambako hawakushudia bao lolote baada ya Leicester City kushindwa kufungana na Chelsea, wakati Manchester United imepata aibu nyumbani wakichapwa 2-0 na Cardiff City, ambao wameshuka daraja.

Southampton wametoka sare ya 1-1 na Huddersfield, wakati Tottenham walitoka sare ya 2-2 na Everton, wakati Watford wamekubali kipigo cha mabao 4-1 nyumbani kutoka kwa West Ham United.

Advertisement

Ligi hiyo imemalizika ambapo kwenye Top Four kuna Man City, Liverpool, Chelsea na Spurs huku Arsenal na Man United zikimaliza kwenye nafasi ya tano na sita. Msimu wa Ligi Kuu England umefungwa kwa kushuhudia wachezaji watatu wakikabana koo kwenye vita ya kuwania Kiatu cha Dhahabu baada ya Mohamed Salah, Sadio Mane na Aubameyang kila mmoja kufunga mabao 22, wakati Aguero amekomea kwenye mabao 21.

 

 

 

Advertisement