Man City kuchukua makombe manne?

Muktasari:

  • Wakati hayo yakiendelea katika FA na ubingwa wa ulaya, hadi kufikia jana Jumapili City ilikuwa inaongoza kwa tofauti ya pointi moja kabla ya Liverpool haijaingia uwanjani kukipiga na Fulham ugenini katika pambano la Ligi Kuu.

MANCHESTER, ENGLAND.HUKO Etihadi harufu ya mataji manne inanukia. Utake usitake. Kuna kila dalili hata kama hautaki kuamini. Wana timu, kocha wa maana, na wanakaribia kuweka historia ambayo haijawahi kuwekwa pale England.

Juzi Jumamosi Manchester City iliigeuzia kibao Swansea ugenini baada ya kuchapwa mabao mawili ya haraka haraka ndani ya dakika 28 lakini ikashinda pambano hilo kwa mabao 3-2 na kutinga nusu fainali za Kombe la FA.

Na sasa, City ambayo tayari imeshachukua Kombe la Ligi kwa kuichapa Chelsea kwa matuta Februari 24 mwaka huu Uwanja wa Wembley ipo katika nafasi nzuri ya kutwaa mataji manne na kuweka historia katika soka la Uingereza. Hakuna timu ambayo imewahi kutwaa mataji manne ndani ya msimu mmoja.

City imetinga katika hatua ya robo fainali Ligi ya mabingwa Ulaya na imep

angwa kucheza na Tottenham katika mechi mbili ikianzia ugenini Wembley mnamo Aprili 9 kabla ya kurudiana Etihad Aprili 17.

Wakati hayo yakiendelea katika FA na ubingwa wa ulaya, hadi kufikia jana Jumapili City ilikuwa inaongoza kwa tofauti ya pointi moja kabla ya Liverpool haijaingia uwanjani kukipiga na Fulham ugenini katika pambano la Ligi Kuu.

Zimebakia mechi nane tu kwa kila timu kumaliza ligi hiyo na endapo City itashinda mechi zake zote basi inaweza kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu. Hii inawaweka City kuwa katika nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa wa England msimu huu.

Mara ya mwisho kwa City kuota ndoto za kuchukua mataji yote manne ilikuwa ni msimu wa 2013/14 wakati ndoto yao ilipokwama Machi 9, 2014 lakini mwishoni mwa msimu ikafanikiwa kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu na Kombe la Ligi.

Chini ya Kocha Mchile, Manuel Pellegrini, City ilifanikiwa kutinga katika hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza mwaka 2014 lakini ikapoteza kwa kuchapwa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Barcelona Februari 18.

City ilifanikiwa kuchukua ubingwa wa Kombe la Ligi kwa kuichapa Sunderland Machi 2, 2014 lakini wiki moja iliyofuata ilitolewa katika michuano ya Kombe la FA na Wigan. Machi 12 Barcelona ikamaliza kazi kwao wakati ilipoiondoa City katika michuano pale Catalunya.

Msimu huu tayari City imevuka Machi 12 na kuna uwezekano mkubwa ikaendelea na ndoto zao za kuchukua mataji manne mpaka Aprili au Mei mwaka huu huku Kocha wa City, Pep Guardiola akitaka kuulizwa uwezekano huo Mwezi ujao.

“Niulize kuhusu hilo mwishoni mwa Aprili na nitakujibu. Nataka kuwapongeza wachezaji wangu na wafanyakazi kwa kufika katika hatua hii. Tayari nimeridhika. Najua watu wengine wataona tumefeli kama hatutachukua mataji matatu au manne. Samahani. Sasa hivi tutapambana kila mechi baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa,” alisema Guardiola.

Kiungo, Bernardo Silva ambaye alifunga bao la kwanza katika pambano dhidi ya Swansea juzi, aliongelea uwezekano wa City kuchukua mataji yote katika michuano yote ambayo wanashiriki kwa sasa.

“Kuna mapumziko ya mechi za kimataifa. Tutajaribu kurudi imara na kupambana kwa ajili ya michuano mingine mitatu iliyobaki. Tunajua kutwaa mataji manne ni ngumu kwa sababu wapinzani wetu ni imara sana. kucheza katika michuano ya Ligi ya Mabingwa inawezekana ni michuano migumu zaidi barani Ulaya, Ligi Kuu nayo ni ngumu na Liverpool inapambana,” alisema Silva.

“Michuano ya FA kitu chochote kinaweza kutokea. Tutajaribu kuwania michuano mitatu iliyobakia kwa asilimia 100 huku tukijua kwamba tunaweza kutwaa yote na tunaweza kushindwa yote. Kila kitu kitatokea ndani ya mwezi mmoja na nusu. Tutajaribu kuwa katika ubora wetu,” alisema staa huyo wa kimataifa wa Ureno.