Man City kitanzini, Guardiola mtegoni

Muktasari:

  • Miongoni mwa masuala yanayochunguzwa ni tuhuma kuwa mmiki wa Man City Sheikh Mansour, kuwalipa mawakala na kuwaweka watu nje ya kanuni katika mikataba kinyume na kanuni za Uefa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) zinataka pande mbili katika mikataba.

Paris, Ufaransa. Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), limesema litaanzisha uchunguzi dhidi ya Manchester City kwa tuhuma ya kukiuka kanuni za usajili.

Mwaka 2014 Man City iliadhibiwa kutokana na kukiuka kanuni elekezi za shirikisho hilo kuhusu ukomo wa matumizi ya fedha za usajili.

Uchunguzi huo mpya unatokana na ripoti zilizofichuliwa na jarida la Der Spiegel la Ujerumani lililodai klabu hiyo ilikiuka kanuni za usajili, lakini ilitumia rushwa kuwazima baadhi ya maofisa wa Uefa.

Shirikisho hilo limekiri uchunguzi wa awali uliofanywa kuhusu Man City, ulipuuzwa hivyo limejiridhisha lazima ufanyike uchunguzi mwingine.

“Uefa itafanya uchunguzi upya kuhusu tuhuma ya matumizi mabaya ya fedha wakati wa usajili kwa Man City, Paris Saint Germain ya Ufaransa na klabu nyingine zinazotuhumiwa kukiuka kanuni,” ilisema taarifa ya Uefa.

Miongoni mwa masuala yanayochunguzwa ni tuhuma kuwa mmiki wa Man City Sheikh Mansour, kuwalipa mawakala na kuwaweka watu nje ya kanuni katika mikataba kinyume na kanuni za Uefa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) zinataka pande mbili katika mikataba.

Wakati huo huo, kocha wa Man City, Pep Guardiola, anatarajiwa kupewa adhabu na Chama cha Soka England (FA) kwa madai ya kumchafua mwamuzi Anthony Taylor aliyechezesha mchezo waliloshinda mabao 3-1 dhidi ya Man United, kwenye Uwanja wa Etihad Jumapili iliyopita.