Man City imeshusha mashine mbili matata!

Saturday July 21 2018

 

LONDON, ENGLAND. MANCHESTER City wameshusha mitambo miwili hadi sasa, Riyad Mahrez na Philippe Sandler na wote hao imewanasa kwa Euro 68 milioni.

Manchester United ishanasa mitambo mitatu hadi sasa, Fred, Diogo Dalott na Lee Grant, ambao wote wamegharimu Euro 82.7 milioni.

Liverpool ndio wamefanya balaa, wameleta mitambo minne, Naby Keita, Fabinho, Xherdan Shaqiri kwa Euro 199.7 milioni. Chelsea wanakwenda mdogomdogo, mtambo walionasa hadi sasa ni Jorginho, aliyewagharimu Euro 57 milioni.

Huko Arsenal kuna mitambo mitano imeshushwa, Lucas Torreira, Bernd Leno, Matteo Guendouzi na Stephan Lichtsteiner na wamegharimia Euro 79 milioni. Tottenham Hotspur wao bado wanasuasua, hawajaleta mtambo mpya, bado wanaamini katika ile ya zamani. Hata hivyo, baadhi ya wachezaji hao wapya bado hawajiunga na timu zao kwa sababu wengine walikuwa na timu zao za taifa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia, hivyo watakuwa na siku nyingi zaidi za kupumzika.

Lakini, hadi kufika Agosti, nyota wengi watakuwa wameshaungana na timu zao na hapo sasa, makocha wa wababe hao wa Top Six kwenye Ligi Kuu England watakuwa na kazi ya kutesti mitambo yao kabla ya kuanza rasmi kwa msimu mpya.

Kocha Unai Emery huko kwenye kikosi cha Arsenal, majaribio ya mwisho kabisa ya kikosi chake atayafanyia kwenye mechi dhidi ya Sevilla itakayopigwa Agosti 4 na baada ya hapo, msimu utakuwa unaanza, ambapo atakuwa na shughuli ya kuwakabili Man City. Pep Guardiola, ubora wa mitambo yake atatesti kwenye mechi dhidi ya Bayern Munich, itakayopigwa Julai 28 na baada ya hapo, atakuwa amepata majibu atoke vipi kwa msimu ujao.

Jose Mourinho, ambaye kwa sasa yupo na kikosi chake cha Man United huko Marekani na wachezaji wengi wakiwa makinda, anaamini hadi Agosti 5 atakuwa na nyota wake wote, ambapo atatesti mitambo yake kwenye mechi dhidi ya Bayern Munich huko mjini Munich, Ujerumani na baada ya hapo kazi itahamia kwenye Ligi Kuu England. Mauricio Pochettino na Spurs yake atatesti mitambo kwenye mechi dhidi ya Girona huko Hispania, Agosti 4, wakati Jurgen Klopp na Liverpool yake atakuwa amefahamu ubora wa mitambo yake kabla ya kuanza kwa msimu mpya wakati atakapoijaribu kwenye mechi dhidi ya Torino, Agosti 7 uwanjani Anfield. Hivyo, ndivyo makocha wa Top Six kwenye Ligi Kuu England watakavyotesti mitambo yao kabla ya kuanza rasmi kwa mchakamchaka wa msimu mpya.

Advertisement