Mamilioni yavunwa mbio za baiskeli

Muktasari:

Sh280 milioni zimekusanywa katika mashindano ya mbio za baiskeli ambazo zina lengo la kuboresha sekta ya elimu nchini. Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda amezindua mashindano ya mbio za baiskeli na kukusanya Sh280milioni kati ya Sh340 milioni zinazotarajiwa kukusanywa kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

Mbio hizo zimepewa jina la 'Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge', yameandaliwa na Kampuni ya Acacia ikishirikiana na taasisi binafsi ya Canada - CanEducate.

Akizungumza katika uzinduzi huo juzi jijini Dar es Salaam, Kakunda alitoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kuchangia mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 3, mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kakunda ambaye alimwakilisha Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo alisema malengo ya mashindano hayo yanaenda sambamba na malengo ya serikali katika kurahisisha mazingira ya utoaji elimu nchini.

 "Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani na kufuta ada za shule na michango ya ziada hadi mwaka jana kumekuwapo na ongezeko la asilimia 44 la uandikishaji wanafunzi wapya wa elimu ya awali, ongezeko la asilimia 33 la uandikishaji wanafunzi wapya wa darasa la kwanza na wanafunzi wapya wanaojiunga na elimu ya sekondari wameongezeka kutoka 366,396 mwaka 2015 hadi 483,216 mwaka 2017", alisema Waziri.

Naye Mkurugenzi wa Acacia nchini, Asa Mwaipopo alisema kwa mwaka jana pekee kampuni hiyo imejenga madarasa na kukarabati mabweni yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 100 wa kike katika Shule ya Sekondari Mwendakulima wilayani Kahama.

"Tangu tuanze kushirikiana na CaEducate mwaka 2011 katika kuboresha sekta ya elimu nchini, Acacia imetumia zaidi ya sh milioni 450 zilizofikia shule 20 na wanafunzi zaidi ya 5000.

Naye Rais wa taasisi ya CanEducate, Rishi Ghuldu alisema kila mwaka taasisi hiyo huwezesha kielimu wanafunzi 270 na kutoa nafasi 11 za udhamini wa masomo ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali duniani.