Mamia wamuaga Mwalusako Dar

Muktasari:

Mwalusako alifariki Jumatatu katika hospitali ya Taifa muhimbili baada ya kuugua kwa muda mrefu.

MAMIA ya waombolezaji wamejitokeza katika msiba wa katibu wa zamani Yanga, Lawrence Mwalusako aliyefariki Jumatatu asubuhi ambapo leo ameagwa kabla ya kusafirishwa kwenda Kyela atakapozikwa

Mwanaspoti Online ambalo lilikuwa msibani hapo toka saa tatu asubuhi, leo Jumatano lilishuhudia wingi wa watu wakijitokeza msibani hapo eneo la Ubungo Kibo jijini.

Moja ya watu waliojitokeza katika msiba huo ni aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF), Leodgar Tenga.

Mwingine aliyehudhuria ni Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Dk Mshindo Msolla ambaye ndiye aliyeongoza mamia ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo waliohudhuria msibani hapo.

Ukiondoa hao, wengine walikuwa ni wachezaji wa zamani kama Thomas Kipese, Monja Liseki, Ally Mayai, Peter Tinno, Kenneth Mkapa na wengineo.

Kwa upande wa TFF, miongoni mwa waliohudhuria ni aliyekuwa mtendaji mkuu wa bodi ya Ligi, Boniphace Wambura.

Pia msiba huo ulihudhuria na wadau mbalimbali wa soka miongoni mwao akiwa ni mchambuzi maarufu wa soka nchini Edo Kumwembe.

Enzi za uhai wake, Mwalusako aliitumikia Yanga akiichezea katika nafasi ya beki wa kati na pembeni, timu ya taifa 'Taifa Stars' lakini pia amewahi kuwa katibu mkuu wa Yanga