VIDEO: Mamia, NextDoor, mashindano, BSS,2018

Muktasari:

Shindano la kusaka vipaji la Bongo Star Search (BSS) msimu wa tisa, baada ya kupata washindi sita kutokea mikoa mitatu, leo limeanza usahili wa kusaka washindi 15 wa Dar es Salaam

Dar es Salaam. Mamia ya vijana wamejitokeza kwa wingi katika shindano la kusaka vipaji la Bongo Star Search (BSS) linaloendelea hivi sasa katika ukumbi wa Nextdoor uliopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yanaanza rasmi leo, yanatarajia kupata washindi 15 baada ya kupata washindi sita kutokea mikoa mitatu.

Shindano hilo limeshapata washindi kutokea mikoa ya Arusha, Mbeya na Mwanza katika kila mkoa imepata washindi sita huku kwa mkoa wa Dar es Salaam litasaka vipaji katika Ukumbi wa Next Door uliopo Oysterbay.

Jaji Mkuu wa BSS, Ritha Paulsen amebainisha mchakato wa kusaka vipaji mikoani ulikuwa ni wenye mafanikio makubwa kutokana na vijana wengi kujitokeza.

Amesema, vijana wamekuwa na hamasa zaidi ya kuimba na kuonyesha uwezo wao kwenye fani hiyo huku akibainisha kuwa majaji wenzake hawakuishia tu kuwapitisha walioimba vizuri ila hata wale waliochemka pia iliwapatia ushauri zaidi.

“Kusema ukweli hamasa imekuwa kubwa kwenye fani hii ya muziki, kitu nilichojifunza  kuwa vijana wana nia ya dhati ya kutaka kujiendeleza kimuziki, na kuwa uwezo wao ni mkubwa ambao unapaswa kuendelezwa.

“BSS imekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia vijana kuona mwanga kwenye fani ya muziki, kwa sasa tumejipanga kuhakikisha tunawainua na kuwafikisha mbali vijana wengi zaidi kwenye fani hii ya muziki,” amesema Madam Rita.

Amewataka washiriki kutoka Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi huku akibainisha kuwa majaji wamejipanga kutumia muda wao mwingi zaidi kusaka na kubainisha vipaji ambavyo ni lazima mshindi wa mwaka huu awe makini.