Mambo ya Tambwe, Ray Sharp kumenoga kinoma

Muktasari:

Tambwe aliyesajiliwa na Yanga akitokea kwa watani wao Simba, anatarajia kufanya sherehe ya ndoa pamoja na mchumba wake, Raiyan ‘Ray wa Tambwe’.

Dar es Salaam. Ule mpando mzima wa sherehe ya ndoa ya mshambuliaji wa Yanga, Mrundi Amiss Tambwe na mchumba wake Raiyan maarufu ‘Ray Sharp au Ray wa Tambwe’ ndiyo tayari kila kitu kimeshapangwa.

Tambwe aliyesajiliwa na Yanga akitokea kwa watani wao Simba, anatarajia kufanya sherehe ya ndoa yake Novemba 9, jijini Dar es Salaam.

Kali zaidi ni kwamba, shughuli za sherehe hizo zitaanza kuanzia Novemba 7, ambapo itakuwa ni upande wa kina mama maarufu kwa jila la Kitchen Part maeneo ya Kariakoo, Novemba 9, kutakuwa na tukio zima la ndoa itakayofanyika upande wa mwanamke Buguruni, Malapa.

Usiku wa tarehe 10, katika maeneo ya Ilala kutakuwa na sherehe ambayo wameipa jina la usiku wa zawadi na baada ya hapo itafuata sherehe yenyewe kubwa na hiyo ni upande wa mwanaume na itakuwa nchini Burundi.

Ray anasema: "Siku ya sherehe hiyo ya Burundi tutaiweka wazi si siku nyingi kwa sababu itakuwa ni sherehe tu hivyo itatategemea kipindi ambacho Tambwe atakuwa katika mapumziko."

Amesema, mambo hayo yanafanyika sasa kwa sababu walipokutana na kuishi pamoja hawakuwa wamefanya sherehe.

Tambwe na Ray wamekutana miaka minne iliyopita na wamefanikiwa kuzaa mtoto mmoja wa kiume anaitwa Ayman.