Mambo ni hatari... Fire
Muktasari:
- Man United kwa sasa ipo chini ya Ole Gunnar Solskjaer, ambaye tangu atue kwenye kikosi hicho kila mchezaji ameonekana kupandisha kiwango chake cha ndani ya uwanja na kucheza kibabe.
MANCHESTER, ENGLAND.NANI anapigwa? Swali kigumu hilo kwenye soka la ndani ya uwanja japo kwenye karatasi, Manchester United haionekani kuleta upinzani mbele ya Lionel Messi na chama lake la Barcelona.
Timu hizo mbili zitakutana kesho Jumatano huko Old Trafford katika mchezo wa robo fainali ya kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakati Man United wakionekana kuwa wepesi tu kwa Barcelona, kiungo wa wababe hao wa Nou Camp, Sergio Busquets alisema wababe hao wa Old Trafford wamekuwa timu tofauti kabisa tangu kocha Jose Mourinho alipobebeshwa virago vyake na kufunguliwa mlango wa kutokea.
Man United kwa sasa ipo chini ya Ole Gunnar Solskjaer, ambaye tangu atue kwenye kikosi hicho kila mchezaji ameonekana kupandisha kiwango chake cha ndani ya uwanja na kucheza kibabe.
Man United wametinga hatua ya robo fainali baada ya kuisukuma nje Paris Saint-Germain na hilo ndilo linalomtisha mchezaji kama Busquets.
“United imekuwa bora sana chini ya Ole Gunnar Solskjaer. Wala hawana shida ya kukuachia ukae na mpira kwa sababu wao wanafahamu wanapoipata tu, basi kitu gani waufanyie mpira huo.
Wako vizuri kwenye mashambulizi ya kushtukiza na mipira iliyokufa, ukifanya kosa kidogo tu, wamekuua,” alisema Busquets.
Wakati masikio na macho ya wengi yakisubiri hilo la kesho huko Old Trafford, mchakamchaka wa mechi za hatua hiyo ya nane bora kwenye michuano hiyo ya Ulaya itashuhudiwa kwa mechi nyingi kibao, ikiwamo hiyo kesho huku Amsterdam, wakati Ajax watakapowakabili Juventus ya Cristiano Ronaldo.
Mechi nyingine za leo, zitawashuhudia Liverpool wakiwa nyumbani Anfield kucheza na FC Porto, huku huko London, Tottenham wakijimwaga kwenye uwanja wao mpya kuwakaribisha Waingereza wenzao, Manchester City katika kipute matata kabisa. Mechi hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Spurs na Man City kumenyana kwenye michuano ya Ulaya. Kuhusu rekodi za Man United na Barcelona ni kwamba timu hizo mbili zimekutana mara 11 kwenye michuano ya Ulaya, ambapo United imeshinda mara tatu, sare nne na kuchapwa mara nne.
Kwa mara ya mwisho kwenye michuano hiyo timu hizo zilikutana fainali uwanjani Wembley, 2011, ambapo Man United walichapwa 3-1 katika mechi iliyoacha kumbukumbu ya aliyekuwa kocha wa Mashetani Wekundu kwa wakati huo, Sir Alex Ferguson kutetemeka mikono. Hiyo kesho unaambiwa mambo ni hatari fire!