Mambo matatu yamrudisha Kaseja Stars

Muktasari:

Umahiri wake katika kuokoa mashambulizi hasa mipira ya ana kwa ana na washambuliaji wa timu pinzani, ile ya krosi na kona pia kupanga safu yake ya ulinzi vikichagizwa pia na uhodari wa kuokoa mikwaju ya penalti ni sifa ambazo zimemfanya Kaseja kuhesabika kama mmoja wa makipa bora hapa nchini katika karne ya 21.

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ inakabiliwa na mechi mbili ngumu dhidi ya Kenya ambazo zitachezwa Julai 28, Dar es Salaam na Agosti 3 jijini Nairobi, Kenya.

Mechi hizo mbili za nyumbani na ugenini ni za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (Chan) zitakazofanyika Cameroon mwakani.

Kuelekea mchezo huo, benchi jipya la ufundi la Taifa Stars chini ya Kocha Etienne Ndayiragije ambalo hivi karibuni liliteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuisimamia timu hiyo baada ya kuvunjwa kwa benchi la zamani chini ya Kocha Emmanuel Amunike, lilitangaza kikosi cha wachezaji 26 kwa maandalizi ya mchezo huo.

Katika kikosi hicho cha wachezaji 26 wa Taifa Stars ambao hivi karibuni wataanza maandalizi ya mechi  dhidi ya Kenya, uteuzi wa kipa wa KMC, Juma Kaseja ndio umeonekana kuwaacha wengi katika mshangao.

Baada ya kukaa nje ya kikosi cha Taifa Stars kwa takribani miaka sita  tangu alipodaka kwa mara ya mwisho mwaka 2012, wengi walihisi kwamba nafasi ya Kaseja timu ya Taifa imefutika rasmi.

Uwepo wa kundi kubwa la vijana walioonyesha viwango vizuri kwenye timu mbalimbali ulionekana kama utazidi kuondoa uwezekano wa Kaseja kujumuishwa katika kikosi cha Taifa Stars.

Baada ya kuvuka milima na mabonde hatimaye Kaseja amerudishwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachojiandaa kuivaa Kenya, akiungana na makipa wengine wawili Aishi Manula na Metacha Mnata.

Lakini pamoja na yote, uamuzi wa kumrudisha Kaseja kwenye kikosi cha Taifa Stars ni sahihi na umekuja katika wakati na mazingira sahihi kulingana na hali inayoikabili Timu ya Taifa kwa sasa.

Spoti Mikiki inakuletea tathimini ya sababu ambazo pengine ndizo zimelishawishi benchi la ufundi la Taifa Stars kumjumuisha Kaseja.

Kiwango bora

Pamoja na ushindani mkali wa namba kwenye kikosi cha KMC anaopata kutoka kwa kipa wa timu ya taifa ya Burundi, Jonathan Nahimana, Kaseja ni miongoni mwa makipa wachache walioonyesha kiwango bora msimu uliopita.

Umahiri wake katika kuokoa mashambulizi hasa mipira ya ana kwa ana na washambuliaji wa timu pinzani, ile ya krosi na kona pia kupanga safu yake ya ulinzi vikichagizwa pia na uhodari wa kuokoa mikwaju ya penalti ni sifa ambazo zimemfanya Kaseja kuhesabika kama mmoja wa makipa bora hapa nchini katika karne ya 21.

Wanasema, namba hazidanganyi na kauli hiyo unaweza kuitumia kuthibitisha ubora wa Kaseja kwa kutazama takwimu zake msimu uliomalizika.

Katika jumla ya mechi 25 alizocheza kwenye Ligi Kuu na Kombe la FA, Kaseja amecheza jumla ya mechi 15 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa huku pia akifungwa jumla ya mabao 13 tu katika mechi hizo zote.

Uzoefu

Sehemu nyingine ambayo Stars itanufaika kutokana na uwepo wa Kaseja ni uzoefu wake ambao ameupata kwa kucheza idadi kubwa ya mechi za mashindano mbalimbali kuanzia yale ya ndani hadi ya kimataifa.

Kaseja amedaka kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa miaka 18 ambayo ndani yake amechezea vigogo vya soka nchini Simba na Yanga ambako alitwaa ubingwa katika timu hizo mbili zote.

Amecheza kwa mafanikio makubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Simba ambayo aliiongoza kutinga hatua ya makundi mwaka 2003.

Kwenye timu ya taifa, Kaseja alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya Tanzania Bara kilichotwaa ubingwa wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati.

 

Ushindani

Idara ya kipa kwenye timu ya taifa kwa muda mrefu kwenye miaka ya hivi karibuni imeonekana kukosa ushindani ambapo kipa Aishi Manula amekuwa hapati changamoto kutokana na kuwaacha mbali kwa uwezo makipa wengine ambao huitwa kikosini.

Kukosa huko changamoto kwa kiasi kikubwa kunamfanya Manula ajisahau na kufanya makosa ambayo huwa yanaigharimu timu lakini mwisho wa siku bado ameendelea kuwa chaguo la kwanza.

Lakini ujio wa Kaseja bila shaka utamsaidia Manula kwani ni kipa wa daraja la juu ambaye amekuwa hafanyi makosa ya kizembe hivyo ni wazi sasa atakuwa makini na ataongeza jitihada ili asipoteze nafasi, pia kuitwa Taifa Stars kutaongeza chachu ya makipa chipukizi kuiga nyayozake baada ya  ndoto zao kuzimwa.