Mambo matano kuivusha Simba

Muktasari:

Hata hivyo kuna kazi ngumu iliyopo mbele yao wanayopaswa kuifanya ili waweze kupata matokeo mazuri pale Lubumbashi ambayo yatawavusha kwani Mazembe wamekuwa moto wa kuotea mbali pindi wanapocheza uwanja wa nyumbani dhidi ya timu yoyote ile.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba leo Jumamosi watakuwa na kibarua kigumu huko Lubumbashi, DR Congo dhidi ya TP Mazembe katika mchezo wa marudiano wa hatua ya Robo Fainali ya mashindano hayo.

Baada ya matokeo ya sare ya bila kufungana kwenye mchezo wa kwanza nyumbani katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba inalazimika kuibuka na ushindi au sare ya aina yoyote ya mabao ili waweze kutinga hatua ya nusu fainali.

Hata hivyo kuna kazi ngumu iliyopo mbele yao wanayopaswa kuifanya ili waweze kupata matokeo mazuri pale Lubumbashi ambayo yatawavusha kwani Mazembe wamekuwa moto wa kuotea mbali pindi wanapocheza uwanja wa nyumbani dhidi ya timu yoyote ile.

Rekodi zinaonyesha kuwa tangu Mazembe ilipofungwa mabao 2-0 nyumbani na Al-Hilal katika mchezo wa hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2009, haikuwahi kupoteza tena mchezo hadi leo hii.

Lakini hiyo haina maana kwamba hakuna uwezekano wa Simba kuwatoa Mazembe kwani lolote linaweza kutokea kwenye mchezo wa soka na wawakilishi hao wa Tanzania wanaweza kuwatupa nje mabingwa hao mara tano wa mashndano hayo.

Simba wanaweza kushtua wengi kwa kuwatupa nje Mazembe lakini hili hilo litokee ni lazima kuna vitu wavifanye ama vingine wanapaswa kuviepuka ili kutimiza ndoto hiyo.

Kwa kulizingatia hilo, Mwanaspoti linakuletea mambo matano ya msingi ambayo Simba wanapaswa kuyafanya ili waweze kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa leo.

1. Mbinu za mchezo

Kila mchezaji wa Simba ndani ya dakika 90 anapaswa kufanyia kazi kwa usahihi maelekezo ambayo benchi la ufundi litamtaka ayafuate kulingana na mpango wa mechi watakaoingia nao.

Pindi timu inapokuwa na mpira wahakikishe haupotei kirahisi kwenda kwa wapinzani lakini pale wanapopoteza, kila mchezaji anapaswa kuhakikisha anahusika katika kuusaka na kutibua hesabu za Mazembe kumiliki na kutengeneza mashambulizi.

2. Kujitolea

Ni jukumu la wachezaji wote watakaopata nafasi kucheza kwa kujitolea pasipo mmoja kumtegea mwingine kwani kwa kufanya hivyo watawapa uhuru wachezaji wa TP Mazembe kucheza kwa uhuru na utulivu wa hali ya juu utakaowafanya wamiliki mpira, kutengeneza nafasi na kufunga mabao kila watakapolikaribia lango la Simba.

Ulinzi wa timu unapaswa kuanzia kwa washambuliaji ambao wanapaswa kuhakikisha hawawapi nafasi mabeki wa Mazembe kuichezesha timu lakini pia kila mchezaji wa Simba anapaswa kuilinda timu dhidi ya mashambulizi ya mipira itokanayo na kona, faulo na krosi ambayo imekuwa tishio kubwa kwao ugenini.

3.Nidhamu ya mchezaji

Kila mchezaji wa Simba anatakiwa kujichunga na kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu na kuepuka kujihusisha na makosa ya utovu wa nidhamu ambao unaweza kumgharimu yeye mwenyewe binafsi na timu.

Mara kwa mara waamuzi barani Afrika wamekuwa wakizibeba timu zinazocheza uwanja wa nyumbani hivyo kosa lolote la utovu wa nidhamu ambalo mchezaji wa Simba atalifanya linaweza kumsababishia adhabu ya kadi ya njano au nyekundu na kuwapa wapinzani wao faulo au penati wanazoweza kuzitumia kufunga mabao.

4. Kutumia nafasi

Simba inapaswa kucheza kwa utulivu na umakini wa hali ya juu katika dakika zote za mchezo.

Umakini hasa unapaswa kuwa kwenye safu yake ya ushambuliaji ambayo inatakiwa kutumia vyema kila nafasi ambayo itapata ndani ya eneo la hatari la Mazembe.

Ikiwa Simba itapata bao la kuongoza mapema litakuwa jambo zuri zaidi kwa sababu ataongeza presha ya wapinzani.

5.Mazoezi ya penati

Inawezekana mechi ya leo ikaja kuamriwa kwa mikwaju ya penati ikiwa timu hizo zitamaliza dakika 90 bila kufungana kama ilivyotokea kwenye mchezo wa kwanza.

Kutokana na hilo, ni lazima Simba wajiandae vizuri katika upigaji wa mikwaju ya penati ili wasiwe kwenye presha kubwa pindi mechi ikilazimika kufika kwenye hatua hiyo kwani jambo hilo halikwepeki kama wamejipanga.