Mambo matano Manji akiyaweka sawa Yanga haishikiki

Muktasari:

Kurejea kwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji kumeamsha hisia za wanachama wa klabu hiyo wakiamini ukata umewakimbia klabuni kwao.

Dar es Salaam.Wanachama na mashabiki waYanga wamenogewa na kujawa furaha baada ya kutangaziwa Mwenyekiti wao Yusuph Manji ameandika barua ya kurejea katika klabu hiyo.

Awali kulikuwa na maneno yakidai kuwa mwenyekiti huyo alikuwa akiwasaidia kimya kimya, lakini baada ya kuandika barua hiyo inaonyesha dhahiri ameamua kurejea kwa moyo mmoja.

Manji alikaa pembeni baada ya kuandika barua ya kujihudhuru mwaka 2017 kutokana na kudai kwamba afya yake haipo vizuri hivyo atashindwa kufanya kazi kwa weledi wa kutosha.

Lakini baada ya kupita mwaka mmoja juzi Jumapili kupitia kwa Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini, Kapteni George Mkuchika, aliwatangazia wanachama wa klabu hiyo kwamba Manji amewaandikia barua ya kurejea rasmi katika klabu hiyo huku akianza kuingia ofisini Januari 15, 2019.

Kurejea kwa Manji kunafanya nafasi yake isizibwe katika uchaguzi unataorajaiwa kufanyika Januari 13, lakini nafasi zingine zilizowazi zitazibwa.

Tajiri huyo sio tu kwamba alijiweka pembeni katika klabu ya Yanga peke yake, bali hadi katika upande wa makampuni yake na ndio maana katika barua ameeleza kwamba tarehe hiyo atarejea katika ofisi zake baada ya kufuata ushauri wa madaktari.

 Kupitia kurejea kwa Manji ndani ya Yanga, tovuti ya Mwanaspoti imeangalia mambo matano akikamilisha baadhi ya vitu basi katika Ligi Kuu kutakuwa patashika mpya.

USAJILI WA KIBABE

Katika suala la kusajili Manji hajawahi kujikweza kutokana na kwamba anapenda kuona timu yake ikifanya vizuri muda wote.

Kipindi ambacho alikuwa yupo madarakani ndani ya kikosi hicho, alikuwa akishusha majembe kutoka nchi yoyote ile kwasababu alikuwa anatoa fungu la kutosha katika usajili wa wachezaji.

Msimu huu wakati unaanza Yanga ilikuwa inapata tabu hata kubakisha baadhi ya nyota wake kutokana na kutokuwa na pesa, hata wale nyota wake waliomaliza mikataba walifanya kuwakopa ili wasaini mikataba mipya.

Kurejea kwa Mwenyekiti huyu huku dirisha dogo la usajili likiwa linakaribia kufunguliwa inamaanisha kwamba Yanga watasajili mchezaji wanayemtaka kwa pesa yoyote ile.

Hivyo kama Yanga iliyokuwa inasajili wachezaji wa kawaida na imerejeshewa neema inamaanisha kutakuwa na moto katika Ligi Kuu.

POSHO NA MISHAHARA YA UHAKIKA

Hakuna siri kwamba Yanga katika upande wa mishahara walikuwa wanaangaliana usoni kutokana na ukata uliopo.

Inasemekana wachezaji wanadai mishahara ya miezi 4, lakini bado walikuwa wanapambana ndani ya uwanja bila kuonyesha matatizo yao.

Kurejea kwa Manji kunatoa taswira kwamba suala la mishahara litakuwa safi kama ilivyokuwa katika kipindi chake huko nyuma.

Wakati huo huo uhakika wa posho nao ukiongezeka zaidi tofauti na hivi sasa mchezaji anakuwa hana uhakika wa posho yake hali ambayo muda mwingine kocha mkuu Mwinyi Zahera analazimika kuzama mfukoni na kutoa chake.

Wakati ambao Manji alikuwa yupo madarakani kabla hajajiuzulu, alikuwa akiwaita wachezaji na kwenda kuchukua mshahara mkononi na baadaye alipowabadilishia muundo wa kuchukua mishahara alichukua akaunti za wachezaji wote na kila mwisho wa mwezi alikuwa akiweka pesa kwa wakati.

Kwa hali hiyo wachezaji walikuwa na uhakika wa kupata mishahara yao tofauti na ilivyokuwa katika msimu uliopita na msimu huu ulivyoanza kwani inasemekana wachezaji hawajapokea mishahara takribani miezi 4.

KULIPA MADENI PESA ZA USAJILI

Lile bakuli linalotembezewa sio kwamba wanaigiza bali ukweli ni kwamba hali ilizidi kuwa mbaya ndani ya klabu hiyo.

Wachezaji wengi wanadai pesa zao za usajili kutokana na kushindwa kumaliziwa mpaka hivi sasa.

Wengine waligoma kusaini mikataba mipya mpaka pale walipomaliziwa za msimu wa mwaka jana, hivyo Manji kurejea kwake anaweza akamaliza  jambo hili na wachezaji kufanya kazi yao kwa weledi uwanjani.

Wakati ambao Manji alikuwa yupo madarakani bega kwa bega na timu hiyo kulikuwa ni ngumu kusikia mchezaji akidai pesa ya usajili kwasababu alikuwa anaweka fungu kwa kila mchezaji ambaye mwalimu anaonyesha kumuhitaji katika kikosi chake.

KUUNGANISHA MASHABIKI

Tayari kuliibuka mpasuko ndani ya kikosi cha Yanga baada ya wanachama kumuhitaji Manji na wengine kumpinga mwenyekiti huyo.

Hivyo kurejea kwake inabidi ahakikishe kwamba mipasuko yote iliyojitokeza kipindi akiwa pembeni anaimaliza ili kuhakikisha anaungwa mkono.

Hili linawezekana kwa Manji kwani amekuwa mtu mwenye sikio la usikivu kutoka kwa wanachama wa Yanga ambao wanampelekea matatizo ya klabu pamoja na yao.

Mashabiki au wanachama wakiwa kitu kimoja wote kwa pamoja wataifanya timu ifanye vizuri kwani watakuwa wanaomba timu ifanye vizuri na sio vibaya.

Hili liliisaidia hata Yanga miaka ya nyuma kufanya vizuri kwasababu Manji alifanikiwa kuwaunganisha wanachama pamoja na kuungwa mkono katika halakati zake za kila siku ndani ya klabu hiyo.

KUWEKA MIKAKATI THABITI YA MAENDELEO NDANI YA YANGA

Yeye akiwa kama mwenyekiti ana nguvu ya kukaa mezani na kamati ya utendaji kisha akatengeneza jinsi ya kujitanua zaidi kibiashara hasa katika upande wa mauzo ya jezi.

Vile vile anaweza akatengeneza mfumo mzuri wa uongozi kuelekea katika uchaguzi na kuifanya Yanga kuwa kampuni na kauchana na kumtegemea mtu mmoja kama ambavyo ilivyo hivi sasa.

Hii ya kufanya Yanga kuwa kampuni inawezekana kwasababu kama akifanya kazi na watu weledi anakila sababau ya kuiacha klabu katika mikono salama hata kama yeye akiondoka.

Mabadiliko hayo yanaweza kuwa kama Simba hivi sasa baada ya kuondoka katika mfumo wa zamani na kuingia katika mfumo wa kampuni.