Mambo 10 yanayochangia majeraha kupona mapema

Muktasari:

Mambo kumi yafuatayo yanaweza kufanywa na majeruhi wa michezo ili kuongeza kasi ya uponaji wa majeraha kwa wakati.

Tunapofanya mazoezi ya kila siku au kushiriki mashindano mbalimbali ni kawaida mwili kupata majeraha madogo madogo, ya kati mpaka makubwa ambayo yanatupa maumivu na homa.

Majeraha hayo yanaweza kuwa ya tishu laini ya wazi yenye mchaniko ama michubuko au kidonda, yanaweza kuwa butu yasiyo ya wazi, ya kuvunjika au kuteguka na pia yakawa mchanganyiko wa vyote.

Mambo kumi yafuatayo yanaweza kufanywa na majeruhi wa michezo ili kuongeza kasi ya uponaji wa majeraha kwa wakati.

Moja, kuacha mara moja kufanya mazoezi au shughuli zozote zinazoweza kusababisha kujitonesa, kujijeruhi au kupata jeraha jipya. Kupumzika sehemu salama na kulala kwa saa 6-8 kwa usiku mmoja.

Mbili, kushikamana na ushauri na matibabu ikiwamo matumizi sahihi ya dawa za mumivu, zakuzuia maambukizi na matumizi ya vidonge vya virutubisho maalumu.

Tatu, utulivu wa kiakili unahitajika kwani shinikizo la kikakili au msongo wa mawazo huathiri kinga ya mwili ambayo ndiyo nguzo muhimu katika kukarabati na kulinda jeraha. Epuka mambo yote yanayokutikisa kiakili.

Nne, kuzingatia maonyo na makatazo yote ikiwamo mitindo mibaya kimaisha kama vile ulevi wa pombe, matumizi ya tumbaku na dawa za kulevya kwani vinaudhoofisha mwili na kuchelewesha uponaji.

Tano, kuzingatia usafi wa mwili ili kuepukana na uvamizi wa vimelea vya maradhi mengine ambayo uwepo wake unadhoofisha mwili kiafya hivyo kuchelewesha uponaji.

Sita, kuwa na mawasiliano ya karibu na wataalam wa afya pamoja na wakufunzi wa michezo lengo ni kupata taarifa muhimu za tatizo lako na ushauri wa haraka pale unapoona viashiria au dalili zisizo za kawaida.

Saba, kula mlo kamili wenye vyakula mchanganyiko kwani mwili unahitaji virutubisho kwa wingi kwa ajili ya seli kufanya kazi ikiwamo kukarabati jeraha.

Virutubisho au viini lishe vinapatikana katika makundi saba ya vyakula ikiwamo protini, wanga, mafuta, mboga, matunda, vyakula vya nyuzi nyuzi na maji.

Wanga ni pamoja na ugali wali, viazi, ndizi na mihogo na vya mafuta ni kama vile mafuta ya mimea na wanyama. Vyote hivi hutupa nguvu na joto.

Protini ni kama vile samaki, kuku, nyama na jamii ya maharage. Vyakula hivi kujenga mwili na hivyo kusaidia jeraha kukarabatiwa na kupona haraka.

Mboga na matunda hutupa maji, vitamini, madini na virutubisho asili ambavyo ni muhimu kwa kujenga kinga imara ya mwili.

Kunywa maji safi na salama angalau lita moja hadi tatu ili kuzuia upungufu wa maji na madini ambao unaweza kusababisha kukamaa misuli hivyo kujijeruhi zaidi. Angalizo, vyakula hivi vinatakiwa kuandaliwa kwa kuzingatia kanuni za afya.

Nane, dhibiti kuongezeka uzito au kunenepa kiholela kwa kuepuka kula vyakula vyenye wanga nyingi, mafuta mengi na sukari nyingi ikiwamo vile vya mtaani, migahawa yakisasa na vya makopo.

Kumbuka uzito au unene mkubwa unaupa mwili shinikizo kubwa na hivyo kuwa katika hatari ya kujijeruhi. Pima uzito mara kwa mara ili kubaini hali hii mapema.

Tisa, anza mazoezi mepesi ikiwamo ya kunyoosha na kulainisha viungo vya mwili endapo tu imethibitisha kitabibu kuwa upo fiti na huna maumivu katika jeraha.

Kumi, fika katika huduma za afya mapema pale atakapoona ushauri na matibabu haukupi matokeo chanya.