Malinzi atoka gerezani na magari matatu, atinga makanisa mawili

Muktasari:

Malinzi na Mwesigwa wamekwepa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukubali kulipa faini ya Sh500,000 kwa Malinzi ambaye alipatikana na kosa la kughushi nyaraka.

Dar es Salaam. Ilikuwa kama filamu wakati aliyekuwa rais TFF, Jamal Malinzi na katibu wake Celestine Mwesigwa walivyowakwepa waandisha wa habari kwa kutoka gerezani Keko na magari matatu.

Malinzi na Mwesigwa walitoka gerezani leo saa 5.14 Asubuhi baada ya kukamilisha malipo ya faini zao Sh500, 000 na Sh 1 milioni walizokubali kulipa jana baada ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwatia hatiani hivyo kuhukumiwa kwenda jela au kulipa faini hizo.

Baada ya hukumu hiyo, Malinzi na Mwesigwa walirejeshwa gerezani la mahabusu Keko kabla ya leo kulipa faini na kuwasilisha risti ya malipo hayo gerezani na kuachiwa huru.

Hali ilivyokuwa Malinzi, Mwesigwa wakitoka gerezani

Saa 5.00 gari ndogo aina ya Mark II nyeupe iliruhusiwa kuingia kwenye geti la magereza na dakika 14 baadae ikatoka ikiwa imewabeba Malinzi na Mwesigwa huku gari nyingine mbili, IST nyekundu na Wish nyeusi zilizowabeba ndugu, jamaa na marafiki zao zikiifuata kutoka eneo la gereza.

Hata hivyo, msafara huo ulipishana ambapo dereva wa gari aina ya Wish alikwenda hadi kanisa la St Joseph Posta na kuzunguka eneo la kanisa hilo kabla ya kutoka saa 05.48 na kisha kuelekea kwenye kanisa la St Peters, Osterbay ambako pia alizunguka eneo la kanisa hilo na kutoka kisha kuelekea nyumbani alikokuwa akiishia Malinzi, Mikocheni.

Katika nyumba hiyo ambayo sasa ni hoteli, gari nyeupe aina ya Mark II ilikuwa ndani ya fensi na gari aina ya Wish nyeusi iliyokuwa kwenye msafara wakati Malinzi na Mwesigwa wakitoka gereza ikiwa imepaki nje ya nyumba hiyo.

Baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki waliojitokeza gerezani kuwachukua Malinzi na Mwesigwa walipishana, wengine wakiingia na kutoka kwenye nyumba hiyo ambayo hata hivyo hawakuruhusu mtu mwingine tofauti na wao kuingia ndani.

Majirani wa eneo la nyumba hiyo walikuwa wamekaa vikundi vikundi kwenye maduka mwili wakijadili kuachiwa kwa rais huyo wa zamani wa TFF.

Habari zaidi soma Mwanaspoti kesho