Malale aanza maandalizi ya Yanga mapema

Muktasari:

Polisi Tanzania ni miongoni mwa timu zilizofanya vizuri katika msimu uliopita wa Ligi Kuu ikiwa chini ya kocha Malale Hamsini.

KOCHA mkuu wa Polisi Tanzania, Malale Hamsini amelazimika kuwaita fasta wachezaji wake kambini na kuendelea na mazoezi baada ya kupisha mapumziko mafupi yaliyotokana na kusimama kwa Ligi kupisha mchezo wa kirafiki wa Tanzania dhidi ya Burundi ambao upo katika kalenda ya FIFA.

Akizungumza na Mwanaspoti, Malale amesema kikosi chake kiliingia kambini mapema kutokana na maandalizi katika mchezo wao dhidi ya Gwambina kuhakikisha wanapata ushindi ambao utawaongezea morali katika mechi yao dhidi ya Yanga.

"Tupo kambini tayari tunajiandaa na mchezo dhidi ya Gwambina tarehe 19, lakini kupitia mchezo huu pia ndio tutajua namna ya kwenda kupambana na Yanga tarehe 22."

Akizungumzia mchezo wao ujao dhidi ya Yanga, alisema ataangalia kucheza mechi moja ya kirafiki ili kuwapa wachezaji wake morali katika mechi hiyo kwani wanahitaji ushindi.

"Kabla ya mechi na Yanga tutacheza mechi moja ya kirafiki, tunataka kuangalia zaidi mbinu zetu zimefikia wapi lakini mbinu hizo tutaanza kuzitumia dhidi ya Gwambina."

Polisi Tanzania inashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 10 katika mechi tano walizocheza, wakishinda mechi tatu, sare moja na na kupoteza mchezo mmoja.