Makuzi ya mtaani kwa Lionel Messi na Ronaldo hayakupishana

Muktasari:

  • Wote walianza kwa kuwa watazamaji na baadaye kuishia uwanjani, binamu ya Cristiano na mtu wake wa karibu, Nuno alikuwa akiichezea Andorinha, siku moja alimwalika kwa ajili ya kuangalia mechi na kumuuliza kama alikuwa tayari kuvaa jezi ya rangi ya bluu na mawingu.

KATIKA toleo lililopita mwandishi, Luca Caioli alimzungumzia namna kipaji cha Messi kilivyoanza kuonekana ingawa kwa wakati huo alipenda zaidi kuchezea gololi na mara chache mpira hadi alipoamua kuungana na kaka zake. Endelea…

Wakati wa sherehe yake ya kuzaliwa akiwa na miaka minne, wazazi wake walimnunulia mpira mweupe ulionakshiwa na madini mfano wa almasi, pengine kuanzia hapo ndipo hamasa ya kupenda soka iliposhika kasi, hadi siku aliyomshangaza kila mmoja.

Baba Na kaka zake walikuwa wakicheza soka mtaani na Messi akaamua kuungana nao kwa mara ya kwanza, wakati wote alikuwa mkononi hakosi gololi lakini safari hii aliamua kuja kivingine.

“Tulishitushwa baada ya kuona kile alichokuwa akikifanya,’’ anasema Jorge. “Hakuwahi kucheza hapo kabla.”

Kuanzia hapo hakukuwa na kurudi nyuma tena, soka ikageuka kuwa sehemu muhimu ya maisha yake yote, ni kama ilivyokuwa kwa Cristiano ingawa wachezaji hao wote walikwama katika mechi zao za kwanza ingawa kuna mfanano mkubwa katika tukio hilo.

Wote walianza kwa kuwa watazamaji na baadaye kuishia uwanjani, binamu ya Cristiano na mtu wake wa karibu, Nuno alikuwa akiichezea Andorinha, siku moja alimwalika kwa ajili ya kuangalia mechi na kumuuliza kama alikuwa tayari kuvaa jezi ya rangi ya bluu na mawingu.

Cristiano alianza mazoezi na baadaye akaamua kubaki eneo hilo, alikuwa ndio kwanza ana miaka sita na miaka mitatu baadaye alikuja kuzawadiwa leseni yake ya kwanza ya michezo namba 17,182 kupitia chama cha soka.

Wakati huo huo alipachikwa jina la utani la Abelhinha yaani nyuki mdogo kutokana na jinsi alivyokuwa akihaha huku na huko uwanjani bila kupumzika.

“Alikuwa na kasi, mwenye mbinu na alicheza vizuri kwa mguu wa kushoto na kulia,’’ anasema Francisco Afonso, Mwalimu wa zamani wa Ronaldo wa shule ya msingi ambaye pia ndiye aliyekuwa kocha wake wa kwanza.

“Kilikuwa ni kitoto chembamba lakini alikuwa mrefu kuwazidi watoto wa umri wake, lakini hakuna ubishi kwamba alijaaliwa kipaji cha asili, hiyo ilikuwa ni sifa yake wakati wote alikuwa mwenye kukimbiza mpira, alikuwa anataka awe wa kwanza kumaliza mchezo,’’ anasema Afonso.

“Alikuwa makini wakati wote pia alikuwa mwenye bidi bila ya kujali alikuwa eneo gani uwanjani, na inapotokea asipate nafasi ya kucheza au akakosa mchezo hilo lilikuwa likimnyima raha,’’ anafafanua Afonso.

Mwaka huo huo, huko Rosario, bibi yake Messi alikuwa kila Jumanne na Alhamisi akienda kuwaangalia wajukuu zake, Rodrigo na Matias wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Grandoli.

Siku moja mchana majira ya kiangazi, Messi aliamua kwenda pamoja nao, kocha wa wakati huo alikuwa ni Salvador Ricardo Aparacio maarufu kama Don Apa ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 80.

Hajawahi kusahau mara yake ya kwanza kumuona Messi ilivyokuwa, “Nilihitaji mtu mmoja zaidi kukamilisha timu,’’ ndivyo anavyosema wakati wote, Don Apa anapoulizwa jinsi alivyobaini kipaji cha staa huyu wa Barcelona.

“Nilikuwa namsubiri mchezaji wa mwisho nikiwa na jezi mkononi mwangu wakati wengine wakipasha misuli moto, lakini mchezaji huyo hakutokea na hapo hapo kulikuwa na hiki kitoto kidogo kikichezea mpira,” anasema Don Apa.

“Hesabu zilikuwa hazichangiki, kwa hiyo nikajiambia liwalo na liwe, lakini sijui kama ataweza kucheza, kwa hiyo nikaamua kwenda kuzungumza na bibi yake ambaye alikuwa mtu wa soka, na nikamwambia, niazime huyu kijana.”

Pia yeye alikuwa akitaka kumuona akicheza uwanjani, aliniambia hilo mara kwa mara akitaka nimpe nafasi nimjaribu, mara kadhaa alikuwa akiniambia kuhusu watoto hawa (Messi na ndugu zake) walivyo na kipaji.

Itaendelea Jumamosi ijayo…