Makosa ya Mabeki yaighalimu Taifa Stars

Muktasari:

Taifa Stars sasa inalazimika kushinda mechi yake ijayo nyumbani dhidi ya Cape Verde ili kubaki katika kinyang’anyiro cha kusaka kufuzu kwa Afcon mwakani

Praia, Cape Verde. Makosa ya safu ya ulinzi ya yameigharimu Taifa Stars baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Cape Verde katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Capo, Mjini Praia.

Cape Verde inayoshika nafasi 65, katika viwango vya ubora wa soka wa Fifa ikiwa nyumbani ilipata mabao yake mawili ya haraka yaliyofungwa na mshambuliaji Ricardo Gomes kabla ya Yanique Tavares kuhitimisha kwa bao tatu.

Mshambuliaji wao, Ricardo Gomes anayekipiga nchini Serbia katika klabu ya Rartizan ndiye alipachika mabao hayo katika dakika ya 16 na 23 akitumia vizuri uzembe wa mabeki wa Stars, David Mwantika na Hassan Kessy, kabla ya Tavares kumalizia la tatu dakika ya 84 kwa shambulizi la kushtukiza.

Katika mchezo huo, Ricardo aling'ara kutokana na kiwango bora alichokionyesha alitolewa nje dakika ya 54, baada ya kupata maumivu.

Washambuliaji Stars wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta walishindwa kabisa kutumia nafasi chache walizopata kupata mabao.

Safu ya kiungo ya Stars iliyoingia kucheza kwa kujilinda walikosa umakini na kuwaacha wenyeji Cape Verde kutawala eneo la kati.

 Kipa wa Stars, Aish Manula alifanya kazi ya ziada kuokoa hatari kadhaa langoni mwake kuepusha aibu ya mvua ya mabao.

Kutokana na matokeo hayo, Cape Verde inapanda mpaka nafasi ya kwanza ya Kundi L iliyokuwa inakaliwa na Uganda 'The Cranes' kwa kuwa na idadi kubwa ya mabao, Lesotho ya tatu na Taifa Stars inashika mkia.

Cape Verde na Uganda wana idadi ya pointi sawa ambazo ni nne. Uganda watacheza mchezo wao wa tatu kesho Jumamosi na Lesotho.

Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo wa marudiano na Cape Verde Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kikosi cha Taifa Stars:

Aishi Manula, Hassan Kessy, Gadiel Michael/ Shomari Kapombe, David Mwantika/ Ally Sonso, Agrey Morris, Abdi Banda, Himid Mao, Mudathir Yahya/ John Bocco, Simon Msuva, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu

Matokeo mengine ya mechi

Cameroon 1 - 0 Malawi

Gabon 3 - 0 Sudan Kusini

Togo 1 - 1 Gambia

Guinea 2 - 0 Rwanda

Ivory Coast 4 - 0 Jamh. Afrika Kati

Angola 4 - 1 Mauritania

Misri 4 - 1 Swaziland