Makonda awaonya vibaka Uwanja wa Taifa

Muktasari:

Tanzania imekuwa ikisifika kwa kuwa na usalama na ndio maana hata Marais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na lile la Afrika (CAF) walifanya ziara hapa

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa tahadhali ya kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu ambao wamekuwa wakifanya uhalifu maeneo jirani na Uwanja wa Taifa kabla, wakati na baada ya Fainali za Afrika kwa vijana zitakazofanyika nchini kuanzia Aplii 14 hadi 28.
Makonda ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ndani ya miundombinu, ulinzi na usalama katika mashindano hayo, alisema kuwa hatokuwa tayari kuona watu wachache waovu wanachafua taswira nzuri ya Tanzania kimataifa kwa kufanya vitendo vya kihalifu wakati wa mashindano hayo.
"Nikiwa kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, niwahakikishie Watanzania kuwa kuanzia mechi ya Taifa Stars dhidi ya Uganda, Jumapili hadi wakati mashindano ya Afrika kwa vijana yatakapomalizika, kutakuwa na ulinzi na usalama wa hali ya juu.
Tanzania imekuwa ikisifika kwa kuwa na usalama na ndio maana hata Marais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na lile la Afrika (CAF) walifanya ziara hapa na watakuja tena hivyo hatutokubali watu wachache watuharibie sifa hii," alisema Makonda.
Makonda alisema kuwa mashindano hayo ni ufunguo kwa Tanzania kupata fursa ya kuandaa mashindano makubwa ya soka duniani hivyo ni lazima itumie vyema mashindano ya Afrika kwa vijana kukaribisha fursa hiyo.