Makonda: Mo Dewji bado hajapatikana

Thursday October 11 2018

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  jana Alhamisi alikanusha taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO Dewji’ huku hadi leo Ijumaa kukiwa hakuna taarifa yoyote ya kupatikana kwa mfanyabiashara huyo.
Awali jana Makonda alitoa kauli ya kupatikana kwa Mo ikiwa ni muda mfupi baada ya kunukuliwa na vyombo vya habari akisema Mo amepatikana na watekaji wamekamatwa.
Hata hivyo Makonda alifafanua kauli hiyo na kusema hajapatikana.
Jana, MCL Digital alipomtafuta Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa jana, hakupatikana lakini Msaidizi wake alithibitisha kupatikana kwake.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Makonda alitoa taarifa ya kukanusha kupatikana kwa Mo Dewji.
Jana Alhamisi asubuhi, MO aliyekuwa akielekea kwenye Hotel ya Colosseum, alitekwa na wazungu wawili na kamanda Mambosasa alieleza kuwashikilia watu watatu.
"Asubuhi ya leo(jana Alhamisi) wazungu wawili walikuwa na gari aina ya Toyota Suff. Kulikuwa na magari mawili, gari moja lilikuwa ndani na lingine lilikuwa nje, gari la ndani liliwasha taa ghafla na lile lililokuwa nje likaingia na kwenda kupaki karibu na gari la MO Dewji lililokuwa limepaki na MO akiwa ndani ya gari hilo,"alisema Mambosasa leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
"Wazungu wawili wakatoka na kumbana MO Dewji baada ya kutoka ndani ya gari lake, na kisha kumpakia katika gari lao aina ya suff na kuondoka naye."

Advertisement