Makocha wanane Ulaya waitaka Stars

Muktasari:

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau alisema makocha hao wanatokea nchi za Hispania, Sweden na wengine wa Ulaya Mashariki.

Dar es Salaam.Makocha wanane wakiwemo wa nchi za Ulaya wamejitosa kuomba nafasi ya kuinoa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

Amunike alisitishiwa mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) muda mfupi baada ya Taifa Stars kutolewa katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) nchini Misri.

Kocha huyo aliyetia saini mkataba wa miaka miwili, ametumikia kwa miezi 10 kabla ya Jumatatu iliyopita TFF kutangaza kusitisha mkataba.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau alisema makocha hao wanatokea nchi za Hispania, Sweden na wengine wa Ulaya Mashariki.

“Hakuna tuliyemjibu kati yao kwa sababu uteuzi wa kocha unafanywa na kamati baada ya kupitia wasifu wa kila aliyeomba,” alisema Kidau.

Pia, Kidau alisema kocha mzawa ndiye atapewa jukumu la kuinoa Taifa Stars kwa mashindano ya Afrika kwa Wanachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (Chan).

“Hatuwezi kupata kocha wa nje hivi karibuni kabla ya Chan, mchakato wa kupata kocha kutoka nje unahitaji muda wa kutosha. Jukumu la kuiongoza Stars atakabidhiwa kocha mzawa,” alisema Kidau. Taifa Stars itaanza na Kenya Julai 27.