Makocha walia ligi ngumu

Dar es Salaam. Michezo ya kwanza ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) imemalizika jana wakati Rhino Rangers ikiikaribisha Mbao FC Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora huku makocha wakitoa maoni yao juu ya ligi hiyo.

Timu ngeni kwenye ligi hiyo, Fountain Gate na African Sports zimeanza vizuri huku Alliance FC na Ndanda FC zilizoshuka daraja kutoka Ligi Kuu zikianza kwa kuchechemea.

Mwanzo mzuri wa timu hizo zinamfanya, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ kusema msimu huu ligi itakuwa ngumu. “Kila timu inataka kuanza vyema ligi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kumaliza nafasi ya juu, zitashuka timu nyingi, hivyo kila mmoja anakuwa muoga,” alisema Malima.

Kocha wa Geita Gold, Fredy ‘Minziro’ alisema kuanza vyema kwa ligi hiyo kunawapa nguvu katika kuendelea kufanya vizuri na kufikia lengo la kucheza Ligi Kuu.

“Bado ni mapema, lakini tunashukuru kwa mwanzo mzuri, kila timu inahitaji ushindi kwenye mchezo wake, hivyo niwaombe mashabiki watulie tutafanya kazi na kuwapa raha,” alisema Minziro.

Hata hivyo kocha wa Alliance FC, Daniel Solonka alisema kichapo walichokipokea ni kutokana na wachezaji wake kushindwa kuelewan dakika 45 za awali, jambo ambalo lilisababisha kufungwa mabao ya haraka.