Makocha wafikiria ushindi mechi ya Azam FC, Ndanda

Muktasari:

  • Hata hivyo katika mechi nne ambazo Ndanda imekutana na Azam katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona tangu mwaka 2014 , wenyeji wameshinda mara mbili na Azam imeshinda mara mbili

Dar es Salaam. Makocha wa Ndanda na Azam wametambiana kuelekea mchezo wao wa leo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara.

Ndanda inaikaribisha Azam leo Alhamis kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa  Nangwanda Sijaona huku ikiwa na rekodi ya kuvutia katika uwanja huo tangu mwaka huu uanze.

Katika mechi nane ambazo Ndandaimecheza kwenye uwanja huo mwaka huu,imepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Ruvu Shooting uliofanyika Januari 7.

Katika mechi hizo nane kwenye Uwanja wa Nangwanda Ndanda iliichapa JKT Tanzania mabao 2-1,ikaifunga Kagera Sugar mabao 2-0,ikashinda bao 1-0 dhidi ya Alliance FC,ikaichapa SIngida United mabao 2-0, ikaifunga KMC mabao 2-0,ikatoa sare ya bao 1-1 na Yanga halafu ikaitandika Coastal Union bao 1-0.

Hata hivyo katika mechi nne ambazo Ndanda imekutana na Azam katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona tangu mwaka 2014 ,wenyeji wameshinda mara mbili na Azam imeshinda mara mbili hivyo kila mmoja ana nafasi ya kushinda mchezo wa leo.

 Novemba Mosi 2014Ndanda iliifunga Azama bao 1-0, Azam ikalipa kwa kuifunga Ndanda bao 1-0 Oktoba 22,2015.Septemba 24,2016 Ndanda iliendeleza ubabe kwa Azam kwa kuifunga mabao 2-1 na Agosti 24,2017 Azam ikalipiza kisasi kwa kuichapa Ndanda bao 1-0.

Kocha wa Ndanda Khalid Adam amesema wako tayari kwa ajili ya mchezo huo  na watapambana kuhakikisha  wanapata ushindi na kujiweka katika nafasi nzuri kwneye msimamo wa ligi.

"Tunachotaka sisi ni uhsindi ili tujiweke vizuri kwenye msimamo kwani bado hatuko salama. Ukiamngalia timu yingi zimekaribiana pointi hivyo ukizembea unashuka chini na ndio maana tunataka tuifunge Azam ili tupate pointi tatu na kuzidi kujinasua na janga la kushuka daraja," alisema Adam.

Kocha wa Azam,Iddi Cheche amesema wamejipanga vizuri kushinda mchezo huo ambao anaamini utakuwa mgumu.

"Najua mechi itakuwa ngumu sana kwani tuko ugenini na wapinzani wetu ni moja ya timu nzuri na ngumu hasa inapokuwa kwenye uwanja wao lakini tumejiandaa vizuri kushinda mchezo huo"alisema Cheche.