Makocha sita vuta nikuvute Chelsea

Muktasari:

  • Chelsea imekata rufaa kupinga kufungiwa kufanya usajili katika madirisha mawili ya usajili, lakini wakati ikisubiria majibu ya rufaa yake, haitaweza kusajili, hivyo itatoka kapa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

LONDON,ENGLAND.IMEFICHUKA kuna orodha ya makocha sita wanaopigiwa hesabu na wababe wa Stamford Bridge wakifukuziwa wakachukue mikoba ya Maurizio Sarri.

Chelsea kigezo chake cha kwanza kwa kocha inayemsaka ni lazima ahakikishie itafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya hata kama inakabiliwa na adhabu ya kufungiwa usajili.

Wababe hao wa Stamford Bridge wapo kwenye mchakamchaka wa kumsaka kocha mpya baada ya Sarri kuhusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na Juventus, na dili hilo linaweza kutokea muda wowote kuanzia sasa.

Frank Lampard, kocha wa zamani wa Juventus, Max Allegri, Kocha Msaidizi wa England, Steve Holland, Kocha wa Ajax, Erik ten Hag na yule wa Wolves, Nuno Espirito Santo pamoja na wa Watford, Javi Gracia wametajwa kwenye orodha hiyo ya makocha wanaosakwa.

Chelsea imekata rufaa kupinga kufungiwa kufanya usajili katika madirisha mawili ya usajili, lakini wakati ikisubiria majibu ya rufaa yake, haitaweza kusajili, hivyo itatoka kapa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Sarri ameisaidia Chelsea kurudi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kumaliza msimu kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu England, lakini pia aliihakikishia zaidi kuingia kwenye michuano hiyo baada ya kubeba ubingwa wa Europa League.

Kwa sababu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni fursa ya kupiga pesa, hivyo Chelsea inataka kocha atakayekuja kwenye kikosi chake kuihakikishia kwamba itakipiga kwenye mikikimikiki hiyo ya Ulaya.

Sarri anaripotiwa ameshakubali mkataba wa miaka mitatu huko Juventus na atakwenda na benchi lake la ufundi kutoka Chelsea.