Makocha matumbo joto robo fainali RBA

Thursday September 17 2020

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Mambo yameanza kunoga Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), ambayo imefikia hatua ya robo fainali kwa vigogo, JKT, Ukonga Kings, ABC, Vijana, Pazi, Oilers, Kurasini Heat na Savio kufuzu.

Mechi za kwanza za robo fainali zitachezwa Septemba 23 kwenye Uwanja wa Bandari, Kurasini.

Pazi itachuana na Oilers, Ukonga Kings itaonyeshana uwezo na JKT, Vijana dhidi ya ABC na Savio itachuana na Kurasini Heat, timu itakayoshinda mechi mbili mfululizo itakata tiketi ya nusu fainali, la sivyo, mshindi wa mechi ya tatu ‘game three’ ndiye atafuzu. Utaratibu huo utatumika pia kwenye mechi za nusu fainali na fainali.

JKT ndiyo timu pekee ambayo ilicheza mechi zote 15 bila kufungwa na kuongoza msimamo ikiwa na pointi 30, ikifuatiwa na ABC, ambayo ilishinda mechi 12 na kufungwa mechi tatu.

Makocha na wachezaji nyota wa timu hizo wameanza kupiga hesabu ya kufuzu kucheza nusu fainali.

Mody Mbwana, kocha wa Pazi alisema licha ya uzoefu wao kwenye historia ya kikapu, watacheza mechi hiyo kwa malengo.

Advertisement

“Tunaiheshimu Oilers, ni timu nzuri, japo kwenye ligi tuliwafunga kwa tofauti ya pointi moja,” alisema Mbwana.

Nyota wa Oilers, Juma Kissoky alisema kwa vyovyote timu yao itafuzu nusu fainali.

“Tumejipanga, japo timu zote tunafahamiana, lakini msimu huu ndoto yetu ni kucheza fainali, Pazi ni timu kongwe kwenye kikapu,” alisema.

Kocha Dennis Funganoti wa Ukonga Kings amewaita kambini wachezaji wake juzi kujiandaa na mchezo na JKT, na kama itafungwa, basi Kings itakuwa timu ya kwanza kuwafunga maafande hao msimu huu.

Advertisement