Makocha hawa EPL wamechoma picha!

Tuesday July 23 2019

 

By Fadhili Athumani

JULAI 4, mwaka huu, wakati akitambulishwa mbele ya wanahabari kuchukua mikoba ya ukocha katika klabu ya Chelsea, Frank Lampard alikuwa mwingi wa furaha.

Tabasamu lake lilionyesha hilo. Nilipomtazama Lampard jinsi alivyokuwa akifurahia kurudi Stamford, tena kama kocha nilijikuta nikitabasamu kwa furaha, mawazo na huzuni, sijui kwa nini. Nilifurahia na kushangilia urejeo wake huku pia nikiwaza itakuwaje itakapofika Desemba 25?

Wakati tukisubiri kushuhudia hatma ya ndoa ya Chelsea na Lampard tuwatupie macho baadhi ya makocha waliokabidhiwa jukumu katika vilabu mbalimbali England, lakini wakajikuta wakikumbana na mfupa mgumu uliowashinda kuutafuna mapema.

ROY HODGSON (LIVERPOOL)

Tayari kuna imani iliyojengeka kwenye Ligi Kuu ya England kuhusu makocha wanaomrithi Rafa Benitez. Katika klabu ya Liverpool, Hodgson alipewa jukumu zito sana. Jukumu la kuweka mambo sawa katika klabu iliyoonekana kuelekea kuporomoka kama si kuharibikiwa.

Uteuzi wa Hodgson ulifanywa na Wamarekani Tom Hicks na George Gillett, wamiliki ambao, tunaweza kusema waliboronga zaidi ya Mike Ashley pale Newcastle, kwani Liverpool katika mikono yao ilipoteza mwelekeo kibiashara, lakini mwishoni walimchukua bosi wa Fulham, Roy Hodgson.

Advertisement

Mara dirisha la usajili likafunguliwa ambapo Hodgson alipewa idhini ya kuimarisha kikosi chake, akafanya usajili wa nyota wa Milan - Jovanovic, Jonjo Shelvey na Danny Wilson, huku pia akifanya usajili wa Joe Cole, Christian Poulsen, Brad Jones na Paul Konchesky.

Akampatia Fabio Aurelio mkataba mpya licha ya kwamba wiki moja kabla ya ujio wake nyota huyo alikuwa tayari amesharuhusiwa kuondoka Anfield. Lakini kati ya nyota wanane aliowasajili, Raul Meireles tu ndiye aliyeonyesha uwezo mkubwa.

Kwa bahati nzuri alifanikiwa kuinusuru Liverpool kutoka aibu ya kushuka daraja, baada ya kuikuta ikiwa katika nafasi ya 19, hii ikiwa ni kutokana na kupata ushindi mmoja katika mechi nane. Liverpool walichapwa na Blackpool, Man United na Everton. Kama hiyo haitoshi, Hodgson pia aliishuhudia timu yake ikipokea kichapo kutoka kwa vibonde wa Ligi Daraja la Pili, Northampton. Yote tisa kumi Hodgson alijikuta akishindwa kujieleza mbele ya wanahabari.

JOE KINNEAR (NEWCASTLE)

Ukiachana na Rafa, Alan Shearer na Kevin Keegan, makocha wengi waliopewa jukumu la kurithi mikoba ya Steve Bruce waliambulia kupambana na hali zao. Haikuwa rahisi kumrithi mtu kama Bruce. Lakini Joe Kinnea, aliamua kujitosa kwenye kamari.

Kinnear (61), ambaye hakuwa na kazi kwa zaidi ya miaka minne alikuwa kocha wa pili, kati ya wanne waliojitosa kumrithi Bruce (2008-09). Ndiye aliyemrithi Kevin Keegan. Lakini badala ya kumakinika na ukocha, alianza kulumbana na mashabiki na wanahabari.

Wakati taarifa zikitoka kuwa Kinnear alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo, Newcastle haikuwa katika nafasi mbaya. Mwezi Februari walikuwa katika nafasi ya 13. Hata hivyo, Magpies ilishuka daraja baada ya timu kukabidhiwa kwa Chris Hughton na Shearer.

DAVID MOYES (MAN UNITED)

Ilikuwa ni dhahiri kuwa kocha yeyote ambaye angekuja kurithi viatu vya Alex Ferguson angepata tabu sana, lakini Man United bado iliamua kumuweka David Moyes majaribuni.

Bila kujiuliza naye akauvaa mkenge. Nakumbuka jinsi Ed Woodward, mtendaji mkuu wa Man United alivyomwagilia sifa wakati akitangaza ujio wake. Haikuishia hapo, baadhi ya mashabiki wa Man United, nao wakadandia treni kwa mbele. Maneno ya Woodward yakawaaminisha kuwa Moyes ni Ferguson mpya. Haraka sana wakatundika bango kubwa katika eneo la Stretford End likisomeka: ‘The Chosen One’.

Akasaini mkataba wa miaka sita wa kukaa Old Trafford, lakini hadi kufikia mwezi Septemba alikuwa tayari anatamani kuondoka. Kulikuwa hakukaliki, hakulaliki. Kilichofuata ni vipigo mfululizo kutoka kwa Swansea, Chelsea, Liverpool, Crystal Palace na Man City.

Mbaya zaidi ni kupoteza mchezo wake wa sita nyumbani dhidi ya West Brom ikiwa ni siku chache tu baada ya kutandikwa 4-1 na Derby County. Kisha kikafuata kichapo cha 3-0 kutoka kwa Liverpool kabla kujikwaa mbele ya mahasimu zao Man City.

Moyes akaonyeshwa mlango wa kutokea kabla ya kumalizika kwa mwezi Aprili. Akaweka rekodi ya kuwa kocha wa tatu ambaye alitimuliwa ndani ya muda mfupi, baada ya miaka 82 katika historia ya klabu hii.

Mskochi huyo akaondoka Old Trafford na kuiacha United, ikiwa katika nafasi ya saba, pointi 13 nyuma ya Arsenal iliyokuwa katika nafasi ya nne. Wakamaliza msimu nje ya top three kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Ligi Kuu ya England (EPL).

ALEX MCLEISH (ASTON VILLA)

“Bluenose scum not welcome”. Kwa tafsiri isiyo rasmi walimaanisha, “Pua ya bluu hairuhusiwi hapa”. Hayo ni maneno yaliyotundikwa katika ukuta wa Bodymoor Heath. Kabla McLeish hajatambulishwa, tayari kulikuwa na maandamano ya kupinga ujio wake Villa Park. Wakati anaondoka Birmingham, mmoja wa viungo wa zamani wa klabu hiyo, Alan Curbishley ambaye alikuwa miongoni waliokuwa wakitajwa kumrithi, alijaribu kumuonya kuhusu yanayomsubiri huko Villa Park, lakini McLeish hakuwa tayari kumsikiliza.

Curbishley anadaiwa kumkumbusha MacLeish juu ya yaliyomkuta Ron Saunders, alipojiunga na Aston Villa, lakini Mskochi huyo hakuwa tayari kupokea ushauri. Jambo ambalo McLeish hakulijua ni uhasama wa jadi uliopo kati vilabu hivi viwili.

Hakujua! Sio kwamba McLeish hakumsikia Curbishley, alimsikia vizuri sana na kumuelewa, lakini nyuma ya kiburi na kujiamini kwake, alikuwepo mtu aliyeitwa Randy Lerner. Huyu ndiye aliyemponza. Kilichofuata ni mfululizo wa filamu ya mvutano kati yake na mashabiki wa Villa katika msimu mzima wa 2011-12.

AVRAM GRANT (CHELSEA)

Mwaka 2007, mashabiki wa Chelsea walikuwa makini sana kuhusu mtu ambaye angeteuliwa kuja Stamford Bridge kumrithi ‘Special One’. Lakini kwa mshangao wa wengi jukumu hilo akakabidhiwa Muisraeli, Avram Grant ambaye haraka sana walimpachika jina la kimajazi, ‘The Old One’.

Haijulikani ni kitu gani kilichomkuna Mrusi Roman Abramovich, kumuamini Muisraeli huyo hadi akamkabidhi majukumu mazito ya ukocha. Grant aliyewasili jijini London kama mkurugenzi wa ufundi akitokea Portsmouth ambako alikuwa ni mkurugenzi wa soka, akapewa kazi ya kumalizia kazi iliyomshinda Jose Mourinho, licha ya kutokuwa na uzoefu huo. Haikuchukua muda akaonyeshwa mlango wa kutokea.

Advertisement