Makocha Simba, Yanga ni kama wanasema!TUSIZOEANE

Friday February 15 2019

 

By THOMAS NG’ITU, MOROGORO

KILE kinachofanywa na Kocha Mwinyi Zahera na vijana Mji Kasoro Bahari, kisha ukaichungulia Simba jijini Dar es Salaam inavyopiga tizi Uwanja wa Boko Veterani, utabaini wazi kuwa, kesho Jumamosi kutakuwa na kazi.

Simba na Yanga zitakutana kwenye pambano lao la 102 tangu kuasisiwa kwa Ligi Kuu Bara mwaka 1965, huku kila moja ikijifua kwa nguvu na kupeana mbinu kwa nia ya kutaka kunyamazishana baada ya dakika 90.

Huko mitaani zile tambo za Yanga ni kama zimezimika baada ya Mnyama kumrarua Mwarabu 1-0 tofauti na kabla ya mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Al Ahly ya Misri kwenye Uwanja wa Taifa.

Namna ambavyo Kocha Zahera anavyowalisha maujuzi nyota wake, huku Mbelgiji naye akiwapa mbinu vijana wake kuna kila dalili mmoja lazima apasuke na ni kama wanaambiana mapema tusizoeane.

MORO NI KONA, KROSI

Mwanaspoti lililoweka maskani yake Chuo cha Kanisa kilichopo Bigwa, Kocha Zahera alionekana kama amepata dawa ya kuwamaliza Simba, baada ya kuwafanyisha nyota wake mazoezi ya kucheza kona na krosi kwa muda mrefu.

Advertisement

Katika mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Highlands, mjini Morogoro, Zahera alianza kwa kuwachangamsha wachezaji wake kwa kuwataka wacheze hangaisha bwege kabla ya kuwapa mazoezi ya mbinu.

Upande wa mazoezi ya mbinu Mkongomani huyo aliukata uwanja kwa kugawa sehemu mbili huku kila goli likiwa na wachezaji watakaocheza kona na wafungaji, ndipo alipotaka umakini zaidi kwenye eneo hilo.

Umakini zaidi alikuwa akiwataka mabeki wake kuzingatia kona fupifupi, ambapo eneo hilo walikuwa wakilicheza kwa umakini kama wakichezewa kona fupi wanatakiwa watoke mabeki wawili, mmoja atamkaba anayeanzishiwa mpira huku mwingine akimkaba wakumuanzishia mwenzake.

Zoezi hilo alionekana kumzingatia vilivyo beki wa kulia Paul Godfrey na kila aliyekosea kocha alikuwa mkali.

Wakati huo huo aligeukia katika upande wa krosi, eneo ambalo umakini uliongezeka huku akimtaka nahodha wake Ibahim Ajibu kupiga krosi zenye uhakika na kuingia ndani ya boksi.

Ajibu alipokosea na kupiga krosi zinaingia kwenye sita ya kipa, Zahera alikuwa akimuelekeza kupiga nje ya eneo hilo huku akisikika akisema ikipigwa hivyo lolote linaweza kutokea.

“Ukipiga nje ya hapa lolote linaweza kutokea na kupata goli, lakini ukipiga ndani kwa kipa akiguswa tu mpira sio wetu,” alisikika akisema huku kauli hiyo ikiungwa mkono na Kocha wa Makipa Juma Pondamali.

Hata hivyo, alipoulizwa na Mwanaspoti kuhusu kutumia aina ya mazoezi, alisema wachezaji wake wamekuwa na makosa mengi kwenye kona na faulo.

“Wachezaji wetu wamekuwa na makosa mengi na hawapendi kupiga mipira ya vichwa wala kukaba, hivyo nimeona nilifanyie kazi hili jambo ili tuweze kurekebisha makosa yetu mapema zaidi,” alisema.

Hata hivyo, kwa upande wa Simba katika eneo la mipira ya kona na faulo ndio imeoneka kufungwa mabao mengi ya aina hiyo, huku mabeki wake wa kati wakisemwa kushindwa kucheza mipira ya namna hiyo.

Simba imefungwa mabao ya kona na faulo katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika hivi karibuni ilivyocheza na AS Vita ya DR Congo na Al Ahly ya Misri.

BANKA SI MTU POA

Kwenye tizi linaloendelea kambi ya vijana wa Jangwani, kiungo Mohammed Issa ‘Banka’ alionekana moto na kung’ara eneo la kiungo kwa uwezo aliouonyesha, kiasi Kocha Zahera alipovigawa vikosi viwili, jamaa alifunika mwanzo mwisho.

Banka alionyesha umahiri kiasi cha kumkuna Zahera na kumtaka zaidi kupambana muda wote anapokuwa uwanjani, hasa katika kukaba.

Hata hivyo, Banka naye hakumuangusha kocha wake kwani aliyafuata maelekezo ya mwalimu huyo ipasavyo.

Urejeo wa Banka katika kikosi cha Yanga unaongeza nguvu kwenye eneo la kiungo ambalo alikuwa anacheza Feisal Salum ‘Fei Toto’, Papy Kabamba Tshishimbi na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

MAKAMBO MTAMKOMA

Naye, straika Herieter Makambo katika mazoezi hayo ni kama aliyekuwa amepewa kazi maalumu ya kucheza na mabeki wa Simba katika pambano hilo la watani kesho Jumamosi.

Katika vikosi alivyovitenga Zahera, lango moja lilikuwa na Klaus Kindoki huku mabeki wakiwa ni Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondani, Paul Godfrey, Gadiel Michael, wakati kati kukiwa na Papy Tshishimbi, Feisal Salum na Ninja na mawinga Mrisho Ngassa na Ajibu mbele kukiwa na Makambo.

Ajibu alikuwa akitumika kama mchezeshaji (playmaker), baada ya kuwa anahangaika kusambaza mipira akitokea pembeni.

Hata hivyo, baadaye alimbadilisha Kindoki katika kikosi cha kwanza na kumpeleka kikosi cha pili kilichokuwa na Banka, Said Makapu, Rafael Daud, Mwinyi Haji, Deus Kaseke, Haruna Moshi, Pius Buswita, Juma Abdul, Gustava Simon kwa kuwapanga ‘zigzaga’ ilikuweza kupambana katika mchezo huo.

Kocha Zahera alisema baada ya kutoka Moro anarejea leo Ijumaa na vijana wake kuendelea kujifua Dar es Salaam kwa mazoezi ya mwisho.

“Tunaenda kufanya mazoezi ya mwisho Dar, tukifika kule ndio tutajua nani aanze kutokana na spidi yake uwanjani,” alisema.

KAGERE, BOCCO MJIPANGE

Licha ya ubora wa washambuliaji wa Simba lakini hilo halijawashtua mabeki wa Yanga.

Beki Dante alisema anajua watu wengi wanaamini Kagere atawasumbua lakini haipo hivyo.

“Tunajua wengi wanaona kama tunakuja kufungwa magoli mengi lakini kila mtu ameshapewa majukumu yake katika mchezo huu hivyo naamini kila kitu kitakuwa sawa,” alisema.

Dante aliongeza katika mchezo huo kama kila mchezaji akifanya kwa usahihi maelekezo aliyopewa, basi wana asilimia kubwa ya kuibuka na ushindi.

ULINZI KAMA WOTE

Kuonyesha Yanga imepania kwenye kambi ya timu hiyo kulikuwa na ulinzi mkali kiasi unaweza kudhani kuna kiongozi maarufu ama supastaa anayelindwa.

Kuanzia kambini hadi mazoezi ulinzi ulikuwa mkali kupindukia. Kwenye Uwanja wa Highlands (Kwa Mzungu) ulinzi umeimarishwa vya kutosha huku ukisimamiwa na Mzee Massawe. Mzee huyo alihakikisha hakuna mtu anayegusa uwanja hadi wachezaji wanapoanza mazoezi.

Wakati huo huo katika Hotel ya Kingsway, bado makomandoo walizidi kutawala nje ya hoteli hiyo huku wakiwa makini na wachezaji wao wasiongee na mtu yeyote yule.

Lakini pia walikuwa wanawata wachezaji wawe na sababu maalumu ya kushuka chini, kama kula tu na sio kitu kingine chochote.

Kingsway ni hoteli ambayo Yanga imekuwa ikiweka kambi yake mara kwa mara inapoingia Mjini Morogoro.

Advertisement