Makocha Alliance, Mtibwa presha juu

Saturday July 4 2020

 

By Clezencia Tryphone

Makocha wa Alliance na Mtibwa Sugar wameonyesha kuanza kuingiwa na mchecheto siku moja kabla ya mechi itakayowakutanisha ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, kocha mkuu wa Alliance FC, Kessy Mziray na mwenzake wa Mtibwa, Zuberi Katwila wametabiri kuwa pambano hilo litakuwa gumu kutokana na nafasi ambayo kila timu ipo kwenye msimamo wa ligi na pia aina ya matokeo yaliyopatikana kwenye mechi ya kwanza baina yao.

“Mchezo huu utakuwa mzuri sana na wenye ushindani hiyo kesho, kutokana na kila timu kuhitaji pointi, maana timu itakayoshinda mchezo huo itakuwa imejiweka katika nafasi nzuri zaidi ya mwenzake

Sisi mechi ya kwanza tuliwafunga, hivyo najua na wao mechi hii ya pili watahitaji kutufunga, lakini sisi tutahakikisha tunapambana kuutumia vyema uwanja wa nyumbani tusipoteze mchezo huo kabisa, tuna mahitaji makubwa sana na pointi tatu katika mchezo huo,” alisema Mziray.

Kocha huyo alisema kuwa katika mchezo wa kesho atawakosa wachezaji Wema Sadoki, Samir Vicent na Martin Kiggi ambao ni majeruhi.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema amewaandaa vyema wachezaji wake kwa ajili ya mechi hilo na jukumu la mwisho ni wenyewe kufanyia kazi kwa vitendo ndani ya uwanja.

Advertisement

“Mchezo huo wa kesho, utakuwa na ushinda mkubwa sana, na kila timu imejiandaa kupata matokeo, cha msingi dakika 90 ndizo zitaamua lakini kwa timu yangu kila kitu kipo sawa,” alisema Katwila.

Katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu uliochezwa mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar walichapwa kwa bao 1-0.

Timu hizo zinakutana katika kipindi ambacho zote ziko kwenye hatari ya kushuka daraja ambapo Mtibwa Sugar wako katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi na pointi zao 37 wakati Alliance walio na pointi 36 wako katika nafasi ya 16.

Advertisement