Makocha AFCON ni tambo na uoga tu

Muktasari:

  • Cameroon walitoka sare ya bila kufungana na Senegal, walishinda bao 2-0 Guinea na 2-1 Morocco.

FAINALI za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zinazoendelea nchini zinaelekea ukingoni baada ya kufikia hatua ya nusu fainali zinazoanza kupigwa leo Jumatano.

Nusu Fainali ya kwanza itazikutanisha Guinea dhidi ya Nigeria mchezo utakaopigwa saa 10 jioni, huku nusu fainali ya pili Cameroon dhidi ya Angola utapigwa saa 1 usiku michezo yote itapigwa Uwanja wa Taifa, jijini Daresalaam.

Kuelekea michezo hiyo, makocha wa timu za Guinea na Nigeria wametambiana kuibuka na ushindi katika mechi zao.

Kocha wa Guinea, Camara Mohammed alisema wamekutana na timu ngumu lakini walipambana mpaka kufuzu hivyo hawaogopi timu yoyote watakayokutana nayo.

“Mchezo wetu dhidi ya Nigeria utakuwa mzuri na wala hatuihofii, tumejiandaa vizuri kushinda na tunatambua kabisa kwamba dunia nzima inatuangalia katika mchezo huu,” alisema.

Naye kocha msaidizi wa Nigeria, Olantusi Baruwa alisema wakati wanakuja kushiriki fainali hizi leongo lao lilikuwa ni kufuzu na kuchukua ubingwa.

“Tulikuwa tunataka tufanye vizuri katika fainali hizi, lengo lilikuwa ni kufuzu na kuchukua ubingwa kwahiyo tumefuzu na sasa tunautaka ubingwa,” alisema.

Aliongeza kupitia fainali hizi wanaamini kabisa vijana wao wengi watapata timu za kucheza Ulaya.

Wakati huo huo, kocha wa Cameroon, Libiih Thomas alisema mchezo wao dhidi ya Angola utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kukamilika.

“Angola sio timu nyepesi wapo kamili kwasababu tunacheza nao inabidi tujipange, hata hivyo tunaamini kabisa tutashinda mchezo huo,” alisema.

Naye Kocha wa Angola, Pedro Goncalves alisema mpaka kufika hatua hiyo wamekutana na mechi ngumu, lakini mchezo wao dhidi ya Cameroon utakuwa mgumu zaidi.

“Unapokuwa unalengo na ukifanikiwa inabidi ujue unafikilia kitu gani, kwa hiyo tunahitaji ubingwa,” alisema.

Aliongeza changamoto kubwa watakayokutana nayo kwa Cameroon ni miili mikubwa na uchezaji wao wa kutumia nguvu.

“Tuliwaona walipocheza na Morocco ni timu inayocheza kwa nguvu nyingi, tutapambana nao kuona tunapata matokeo katika mchezo huu,” alisema.

Angola wamefuzu baada ya kuifunga Uganda 1-0, walifungwa 1-0 dhidi ya Nigeria na kuifunga Serengeti Boys bao 4-2.

Cameroon walitoka sare ya bila kufungana na Senegal, walishinda bao 2-0 Guinea na 2-1 Morocco.

Wakati Nigeria waliifunga Tanzania bao 5-4, 1-0 Angola na sare ya bao moja na Uganda na kwa upande wa Guinea walifungwa bao 2-0 na Cameroon, Senegal bao 2-1 na waliifunga Morocco 1-0.