Makocha 7 waitaka Yanga SC

YANGA imemfuta kazi Kocha wake Mkuu, Luc Eymael huku sababu nzito zikifichuka na msaidizi wake, Boniface Mkwassa amewaambia viongozi; “Nipeni timu.”

Mwanaspoti lilimtafuta Mkwasa ambaye alisema yupo tayari kurejea Yanga kwani, ametoka nayo mbali licha ya kuondoka kwenye benchi hilo kutokana na tofauti zake na Eymael.

Alisema mkataba wake na Yanga unamalizika mwezi ujao na amepinga madai ya Eymael kwamba, hakuwa akimsaidia kwa lolote kwenye benchi la ufundi.

“Nilikuwa nasimamia mazoezi na kutafsiri kwa wachezaji na nilishangazwa sana na madai ya Eymael kwamba, sina msaada katika timu. Nikiwa kocha mwenye heshima zangu nisingeweza kuendelea kuwa na kocha, ambaye hatambui mchango wangu,” alisema.

WANAOTAJWA

Baada ya Eymael kufurushwa hadi jana mchana kulikuwa na kundi la makocha waliokuwa wakitajwa kwamba, wanaweza kuinoa Yanga. Kuna makocha saba ingawa ni wawili tu ndio wanaonekana kuwa na nguvu zaidi.

Makocha hao ni Hitimana Thiery na Mecky Maxime ambao, mmoja anaweza kutua kama kocha msaidizi na mchakato wa hilo tayari ulishaanza mapema.

Lakini, habari za ndani zinasema hata kabla ya kumng’oa Eymael, ambaye Mwanaspoti kama lilivyokudokeza alikuwa akisubiri muda ufike tu, alishapewa sharti la kuchagua msaidizi mmoja kati ya Maxime na Hitimana.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wanaopewa nafasi ni George Lwandamina (Kocha Mkuu wa Zesco) na Florent Ibenge wa AS Vita ya DR Congo. Hata hivyo, kuna baadhi ya mabosi na wanachama wa Yanga wanaamini hata kocha wao wa zamani, Hans Pluijm na Patrick Aussems wanatosha kuivusha klabu hiyo.

Habari kutoka korido za Jangwani zinaeleza kuwa, Lwandamina bado anakubalika sana ingawa kumekuwa na uhusiano wa karibu kati ya vigogo wa GSM na Ibenge, ambaye amehusika katika mchakato wa Yanga kuwanasa mastaa wapya kutoka DR Congo. Mastaa hao ni Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe ambao ni tegemeo ndani ya AS Vita.

Hata hivyo, mabosi wa Yanga jana hawakuwa tayari kueleza kwa undani kuhusu mchakato wa kumnasa kocha mpya kwa madai kwamba, wako bize kurejesha timu Dar kutoka Iringa.

Katika Mwanaspoti toleo la Ijumaa Julai 24, mwaka huu, tulieleza sababu saba ambazo zitamng’oa Eymael Jangwani.

Pia, lilieleza namna mabosi wa Yanga walivyokuwa wamejipanga kumfyeka kama angepoteza mchezo dhidi ya Mtibwa ulioisha kwa sare ya bao 1-1 ama ule wa Lipuli ambao hata hivyo, alishinda.