Makipa Yanga wakaa mkao wa kula

Muktasari:

  • Karibu kila timu sasa inajiandaa kwa ajili ya kurejea katika ligi baada ya Serikali kutangaza Juni Mosi kuanza kwa michezo baada ya kusimama kwa muda

KOCHA wa Makipa wa  Yanga Peter Manyika amesema hana shaka na walinda mlango wake watakaporejea mazoezini.
Kauli hiyo ya Manyika imekuja siku chache baada ya mipango ya kurejesha Ligi Kuu na mashindano mengine ya soka nchini kurejea baada ya kusimamishwa  na serikali tangu Machi 17 ikiwa ni hatua za kukabiliana na virusi vya corona.
Akizungumza na Mwanaspoti, Manyika anasema, hana Shaka na makipa wake kutokana na kujitambua kwao na kujua wao wanahitaji kufanya nini katika wakati gani.
Anasema, programu alizowapa katika kipindi chote hicho ambacho ligi ilikuwa imesimama anaamini wamezifanyia kazi na wako tayari kwa ratiba zilizo mbele yao.
"Makipa wangu kwanza wanajitambua, na kujua nini wanatakiwa kukifanya katika timu yao, sitapata shida sana.
Mimi, kesho narejea Dar es Salaam ili nijue kinachoendelea baada ya Serikali kuruhusu michezo kuendelea," anasema
Aidha Manyika anasema,mazoezi ambayo wachezaji walikuwa wanayafanya ni ya kujenga mwili hivyo watakaporejea anawapa ya mbinu ili kurejea katika viwango vyao vya awali.
Yanga wanatarajia kuanza mazoezi ya pamoja kesho jijini na kabla ya mazoezi wachezaji wote watafanyiwa vipimo
 Manyika alijiunga na Yanga kabla ya msimu huu kuanza akichukua mikoba ya Juma Pondamali ambaye alionyeshwa mlango wa kutokea