Makipa Ligi Kuu ni vita

Muktasari:

Hadi sasa, kipa wa Azam FC, David Kisu hajaruhusu bao hata moja msimu huu.

Dar es Salaam. Wakati kasi ya washambuliji kufumania nyavu ikiwa bado haijaanza kuchanganya, ushindani wa walinda mlango katika kusaka tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu msimu huu umeanza mapema.

Licha ya raundi za ligi zilizochezwa kuwa nne hadi sasa, kundi kubwa la makipa limeonekana kuonyesha kiwango bora katika mechi za mwanzoni na kusababisha kutoruhusu nyavu zao kutikiswa katika idadi kubwa ya michezo.

Kutokana na idadi ya michezo ambayo kipa hajaruhusu bao katika lango lake kuwa ndiyo kigezo kikuu kinachotumika kuamua mshindi wa tuzo ya kipa bora wa msimu, raundi nne za mwanzo zimeanza kutoa ishara kuwa huenda safari hii kukawa na ushindani mkali wa tuzo hiyo.

Katika raundi nne za mwanzo za Ligi Kuu msimu huu, kipa wa Azam FC, David Kisu ndiye anayeongoza kwa kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao, amecheza dakika 360 dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union, Prisons na Mbeya City.

Kisu anafuatiwa kwa ukaribu na wenzake Aron Kalambo wa Dododoma Jiji FC, Dan Mgore wa Biashara United na Metacha Mnata (Yanga), ambao kila mmoja amecheza kwa dakika 270 bila bao.

Wakati Mgore akicheza mechi dhidi ya Gwambina, Mwadui FC na Ruvu Shooting bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa, Mnata hajaruhusu bao katika mechi dhidi ya Mbeya City, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar wakati Kalambo hajafungwa dhidi ya Mwadui FC, JKT Tanzania na Coastal Union

Ukiondoa makipa hao, Aishi Manula (Simba), Ramadhan Chalamanda (Kagera Sugar), Abuutwalib Mshery (Mtibwa Sugar), Geophrey Mkumbo (Polisi Tanzania) na Bidii Hussein wa Ruvu Shooting, kila mmoja amecheza mechi mbili bila kufungwa.

Kinara makipa, David Kisu alisema lengo lake ni kuisaidia timu yake kufanya vyema msimu huu.

“Siri ya mafanikio ni kujituma na kufuata kile ninachoelekezwa, lakini kubwa zaidi ni neema za Mungu kwa sababu ndiye kila kitu.

“Nahitaji kufanya makubwa zaidi, lakini lililo bora ni kuisaidia Azam FC katika ligi na mashindano ya kimataifa,” alisema Kisu.

Kwa upande wa Kalambo, alisema juhudi za kitimu ndizo zinambeba.

“Nadhani ni matokeo ya juhudi za pamoja kama timu na kila mtu anatimiza vyema majukumu yake ndiyo maana tumecheza mechi tatu kati ya nne bila kuruhusu bao. Ni ndoto zangu kufanya vizuri zaidi,” alisema Kalambo.