Makinda waliotisha robo fainali Ligi ya Mabingwa

Muktasari:

Makinda mafundi wa mpira waliotinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hakuna ubishi, Marcus Rashford moja kati ya mazao bora kabisa kutoka kwenye akademia ya Manchester United kwa miaka ya karibuni.

DROO ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imepangwa hivi karibuni na kuleta mechi matata kabisa zinazowafanya mashabiki wa soka hilo la Ulaya kuvisubiri kwa hamu vipute hivyo.

Hebu cheki, Manchester United itakipiga na Barcelona, Liverpool itacheza na FC Porto, Juventus itatoana jasho na Ajax na Tottenham itakuwa na shughuli na Waingereza wenzao, Manchester City.

Wakati mashabiki wakisubiri mechi hizo, ambapo timu itakayoshindwa kupata matokeo katika mechi mbili itakuwa ametupwa nje ya michuano, kwenye vikosi vyote vinane kuna makinda hao wapo vizuri kinoma na wanatazamwa kama silaha za kuzifikisha nusu fainali timu zao. Hawa hapa makinda hao ambao wanaolishikilia soka la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu hasa baada ya sasa kufika kwenye hatua ya nane bora.

Phil Foden- Man City, miaka 18

Kinda wa Kingereza mwenye umri wa miaka 18, Phil Foden anayekipiga huko kwenye kikosi cha Manchester City ni mmoja kati ya wachezaji wenye umri mdogo waliopo kwenye ubora mkubwa kabisa wa soka la huko Ulaya kwa sasa.

Kocha Pep Guardiola amekuwa akimtambua Foden kuwa moja kati ya silaha zake matata kabisa kwa siku za baadaye katika kikosi hicho cha Man City. Katika mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Schalke, Foden alifunga bao lake la kwanza kwenye michuano hiyo akiwa na Man Cityt. Jambo hilo lilimfanya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuifungia Man City kwenye michuano ya Ulaya akifanya hivyo akiwa na umri wa miaka 18 na siku 288. Si jambo litakaloshangaza kama Foden akianzishwa kwenye mechi ya robo fainali dhidi ya Tottenham Hotspur.

Matthijs de Ligt– Ajax, miaka 19

Beki wa Kidachi, Matthijs de Ligt jinsi alivyolishika soka la Ulaya na kusakwa na timu mbilimbali wala huwezi kudhani kama umri wake ndio kwanza ni miaka 19 tu.

Kinda huyo alicheza kwa kiwango kikubwa sana kuisaidia timu yake ya Ajax kuivua ubingwa Real Madrid na kuitupa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kucheza kwa ubora usioshuka kwenye kikosi hicho cha Ajax akaifanya kuwa na ngome imara kumezifanya klabu nyingi zikiwamo Barcelona na Juventus kuingia kwenye vita ya kuisaka huduma yake.

Ajax itaikabili Juventus kwenye hatua ya robo fainali na De Ligt huenda akatumia nafasi hiyo kuwavuruga kabisa wababe hao wa Italia wanaotoka udenda kuifukuzia huduma yake.

Trent Alexander-Arnold– Liverpool, miaka 20

Staa wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold kwa mbali sana amewaacha wengine kwenye orodha ya mabeki wenye umri mdogo wanaotamba kwenye soka la Ulaya msimu huu. Mchezaji huyo akiwa na umri wa miaka 20, Trent ameonyesha ukomavu mkubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kumfanya Kocha Jurgen Klopp kutokuwa na mashaka juu ya huduma yake. Beki huyo amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu tangu alipoanza kuchezea kikosi cha wakubwa cha Liverpool na mwaka 2017 na 2018 alichaguliwa kuwa mchezaji bora kijana kwenye kikosi hicho cha Anfield. Aliichezea England katika ngazi zote za timu ya vijana kabla ya kujumuishwa kwenye kikosi cha wakubwa kilichokwenda kwenye Kombe la Dunia 2018 huko Russia mwaka jana.

Atakuwapo uwanjani kwenye mechi ya robo fainali na chama lake la Liverpool litachuana na FC Porto.

Rodrigo Bentancur– Juventus, miaka 21

Tangu alipojiunga na Juventus, Julai 2017, Rodrigo Bentancur mwenye umri wa miaka 21 kwa sasa amekuwa kwenye kikosi bora akiwa kinda matata kwenye kikosi hicho cha Turin. Kwenye kikosi cha Juventus kilichosheheni mastaa watupu kwenye sehemu ya kiungo, lakini kinda huyo anaibuka na kupata nafasi kwenye kikosi hicho na kucheza mechi kibao. Umbo lake limemfanya Bentancur kuwa na nafasi kubwa ya kucheza kwenye kikosi huku uwezo wake wa kutumia miguu yote miwili imemfanya awe mchezaji tishio zaidi. Anaweza kucheza kiungo ya kukaka, kiungo ya kati, winga au kiungo mshambuliaji na hivyo kumfanya Bentancur kuwa mmoja kati ya makinda watakaobamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Juventus inategemea kupata huduma bora kabisa kutoka kwa Bentancur katika mechi yake ya robo fainali dhidi ya Ajax.

Ousmane Dembele– Barcelona, miaka 21

Winga wa Barcelona, Ousmane Dembele ni mmoja kati ya makinda wenye vipaji vikubwa sana wanaotamba kwenye soka la Ulaya kwa sasa.

Barcelona itacheza dhidi ya Manchester United kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Dembele ni mmoja kati ya wachezaji tishio kwenye mechi hiyo na mashabiki wa Man United wanafurahia baada ya kusikia huenda asicheze kwa kuwa majeruhi.

Kinyume cha hapo hali ingekuwa ngumu zaidi katika kumkabili Lioel Messi huku kuna Dembele pia.

Staa huyo wa Ufaransa amekuwa na uwezo mkubwa wa kuwachomoka mabeki linapotokea suala la kukabwa ana kwa ana, Dembele yupo vizuri sana.

2. Marcus Rashford- Man United, miaka 21

Hakuna ubishi, Marcus Rashford moja kati ya mazao bora kabisa kutoka kwenye akademia ya Manchester United kwa miaka ya karibuni.

Kiwango chake bora anachokionyesha ndani ya uwanja kinafanya suala la kuwindwa na timu vigogo kama Real Madrid kuonekana kuwa la kawaida tu. Kwenye mechi ya hatua ya 16 bora ambapo Man United iliitupa nje PSG, Rashford alifunga kwa penalti muhimu kabisa katika mechi hiyo na kuisaidia timu yake kusonga mbele. Amefunga mabao 26 kwenye mechi 104 alizochezea Man United, huku akifunga mara sita pia katika mechi 31 alizochezea Timu ya Taifa ya England na umri wake wa miaka 21 hilo limeonyesha Rashford si mchezaji wa mchezomchezo.

Eder Militao- FC Porto, miaka 21

Beki wa Kibrazili, Eder Militao ni kati ya makinda matata kabisa wanaotamba kwenye soka la Ulaya msimu huu na kinachoelezwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, tayari ameshakubali kujiunga na Real Madrid mwishoni mwa msimu. Kwenye mauzo yake, Porto itavuna Euro 50 milioni.

Iwe kwenye beki ya kulia au kati, Militao amekuwa na uwezo mkubwa wa kuzimudu nafasi hizo na ndio maana panga pangua amekuwa hakosekani kwenye kikosi cha FC Porto hadi sasa kilipofikia hatua ya robo fainali katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo timu yake itamenyana na Liverpool.

Eder ni kinda mwenye kipaji kikubwa sana.

Juan Foyth– Tottenham, miaka 21

Beki kinda wa Kiargentina, Juan Foyth ameibukia na kuwa juu kweli kweli huko kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur akionekana kuwashika akiwa ndio kwanza na umri wa miaka 21 tu. Kocha Mauricio Pochettino ameamua kumchukua kinda huyo na kumpa nafasi kwenye kikosi chake kabla ya kuanza kwa hatua ya mtoano mwezi uliopita. Foyth litakuwa chaguo mwafaka kwenye kikosi cha Spurs kwenye mechi za robo fainali dhidi ya Manchester City.

Frenkie de Jong– Ajax, miaka 21

Msimu ujao atakuwa kwenye kikosi cha Barcelona. Kiungo wa Ajax, Frenkie de Jong mmoja kati ya makinda waliolikamata soka la Ulaya kutokana na kiwango chake bora kabisa cha uwanjani. Kwenye mechi zote mbili dhidi ya Real Madrid kwenye hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, De Jong aliwatuliza viungo wa Los Blancos akiwamo Luka Modric.

Akiwa na umri wa miaka 21 tu, lakini De Jong ni balaa zito, akicheza kwenye kiungo ya chini, fundi na anatumia nguvu pia. Uwezo wake wa kuseti mipango akitokea kwenye sehemu hiyo ya katikati ya uwanja na hicho ndicho kilichoifanya Barcelona kwenda kumsajili haraka na mwishoni mwa msimu atajiunga kwenye timu yao.